Na Winfrida Nicolaus
Imeelezwa kuwa unapohitaji kuwa na ng’ombe bora wa maziwa na azalishe maziwa mengi kwa tija ni lazima kuzingatia uzao wake hivyo kama mfugaji ni lazima kutafuta Ng’ombe mzuri ambae ana sifa za kuzalisha maziwa vizuri.
Maelezo hayo yametolewa na Meneja katika Idara ya Mashamba ya Kisasa ya Mfano Kitengo cha Mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Bw. Farid Chamkwata wakati akizungumza mubashara na SUA Redio kutoka Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro.
Amesema ukichukua wanyama kwenye sehemu ambayo kuna wanyama wazuri au Uzao wa kwanza (Pure Breeding) una uhakika mkubwa wa kuja kuzalisha watoto watakaokuwa ni bora na wenye manufaa kwenye shamba.
“Tumekuja kwenye Maonesho haya ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa ajili ya kuionesha jamii Dume Bora la Ng’ombe wa maziwa lakini pia ushauri kwa wafugaji wa ng’ombe ili kuzingatia upandishaji wa wanyama wao kwa mbegu zilizo Bora ili zilete ufanisi mzuri katika soko la mazao hasa Soko la Mazao ya maziwa”, amesema Chamkwata.
Bw. Chamkwata ameongeza kuwa njia nyingine ya kupata Dume bora la Ng’ombe wa Maziwa ni mfugaji kuwa na malisho ambayo yamezalishwa kitaalamu pamoja na kuzingatia namna sahihi ya ulishaji hivyo ameitaka jamii kutembelea banda la SUA kwa lengo pia la kujifunza namna Bora ya kufuga ndama wa maziwa pamoja na jike bora la maziwa linavyokuwa.
0 Comments