SUAMEDIA

Wafugaji watakiwa kutenga chumba cha wagonjwa kuepuka kusambaza magonjwa

Na: Farida Mkongwe

Wafugaji wa kuku nchini wametakiwa kutenga chumba au sehemu maalumu ya kuuguzia kuku wagonjwa ili kuepuka kusambaa kwa magonjwa yanayoambukiza ambayo yanamsababishia mfugaji kupata  hasara.


Afisa Kilimo kutoka Idara ya Tiba ya Mifugo na Afya ya Jamii SUA Bibi. Enesa Raphael Mlay (kushoto) akitoa maelezo ya ufugaji kuku kwa baadhi ya watu waliofika kwenye banda hilo. Picha na Nicholus Roman

                    

Kauli hiyo imetolewa Agosti 3, 2023 na Afisa Kilimo kutoka Idara ya Tiba ya Mifugo na Afya ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Bibi. Enesa Raphael Mlay wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane mjini Morogoro.

Bibi. Enesa amesema banda la kuku linatakiwa liwe na vyumba vitatu, kuwepo na chumba cha kuku na mama kuku yaani kuku na vifaranga ambavyo vinahitaji usalama na joto kutoka kwa mama yao, chumba cha kuku wakubwa yaani majogoo na matetea pamoja na wale wanaotaga na chumba cha wagonjwa.

Umuhimu wa hiki chumba cha wagonjwa ni kupunguza kusambaza magonjwa pale kwenye chumba ambacho wametoka, kwa hiyo ugonjwa ambao umempata kuku mmoja ni vyema ahamishwe apelekwe kwenye wodi ya wagonjwa ili kule sasa aweze kupata dozi kamili pamoja na chakula ili afya yake iweze kuimarika, amesema Afisa huyo.

Lakini faida nyingine ya hiki chumba cha wagonjwa ni kwamba hata yule mtu ambaye anahudumia basi tunashauri atakapofanya usafi basi chumba cha wagonjwa kiwe cha mwisho ili kwamba na yeye nguo zake, viatu vyake na mikono yake isiwe sababisho ya kwenda kuhamisha magonjwa kwa hawa kuku wengine, amesisitiza Bibi. Enesa.

Katika hatua nyingine Afisa Mifugo huyo kutoka SUA amewashauri wafugaji kuzingatia chanjo na kuwanunuliwa kuku vitamini zinazouzwa katika maduka ya mifugo hasa katika kipindi hiki cha kiangazi ambapo majani mengi yanakauka.

Tunashauri katika kipindi hiki cha kiangazi ni vizuri uende kwenye duka la madawa ya mifugo ununue vitamini ambayo utawawekea kuku kwenye maji ya kunywa ili wasije wakapata ule ugonjwa ambao kuku hawaoni na macho yanavimba, macho yakiathirika ina maana hawezi kula na vifo vinakuwa ni vingi, amesema Bibi. Enesa.

 




Post a Comment

0 Comments