SUAMEDIA

Wakulima washauriwa kutumia majani ya Juncao kwa malisho ya mifugo

 Na: Farida Mkongwe

Wakulima na Wafugaji nchini wameshauriwa kupanda na kuyatumia majani aina ya Juncao kwa ajili ya malisho ya mifugo kutokana na majani hayo kuwa na virutubisho vingi ukilinganisha na majani mengine .




Ushauri huo umetolewa Agosti 3, 2023 na Mtaalamu wa Malisho kutoka Idara ya Shamba ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Kampasi ya Solomon Mahlangu Melkiard Tairo wakati akizungumza na SUAMEDIA katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro.

Bw. Tairo amesema majani ya Juncao yameonekana kuwa na faida nyingi kwa mifugo kutokana na virutubisho vilivyomo kwenye majani hayo na pia yana uwezo wa kukua haraka na kuvumilia ukame na hivyo kupunguza changamoto za malisho wakati wa kiangazi .

Haya ni majani yanayotumika kwa pande mbili upande wa mifugo na pia yanatumika kwenye uzalishaji wa uyoga katika kitalu na yanakuwa makubwa zaidi kuliko majani tembo (elephant grass)na yanaweza yakakua zaidi ya mita 8, ni majani yenye faida sana kwa sababu pia yanazuia mmonyoko wa ardhi, amesema Mtaalamu huyo.

Katika hatua nyingine Bw. Tairo amewashauri wakulima na wafugaji kuandaa malisho yatakayotumika wakati wa kiangazi kwa sababu kipindi hicho kunakuwa na ukame hivyo kusipokuwa na malisho ya kutosha yaliyohifadhiwa wafugaji wengi upata shida ya kutafuta malisho .

Tunashauri sana wakulima waweze kujikita katika suala hili la kuhifadhi majani kwa ajili ya kiangazi maana ukiangalia misimu ya sasa hivi kiangazi ndio kinakwenda muda mrefu sana kwa hiyo tunapaswa kuhifadhi majani ya kutosha kwa sababu ya mifugo yetu, ameshauri Mtaalamu huyo.

  

          



Post a Comment

0 Comments