SUAMEDIA

Wanafunzi Zanzibar watakiwa kusoma programu zenye mahusiano na Uchumi wa Bluu SUA

 

Na: Asifiwe Mbembela 

Wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa shule ya Sekondari Lumumba na  Ben Bella kutoka Zanzibar wameelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatoa programu mbalimbali zinazoendana na Sera ya sasa ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayohusu uchumi wa bluu.


Maelezo hayo yametolewa Agosti2, 2023 na Bi. Zahra Majili, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule za Ben Bella na Lumumba zilizopo Mjini Magharibi katika Kisiwa cha Ugunja, Zanzibar katika ziara maalum iliyofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa SUA wanaoshiriki Maonesho ya 4 ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar 2023 yanayoendelea Viwanja wa Maisara.

Bi. Zahra Majili amewaambia wanafunzi wa shule hizo kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakidhani SUA inafundisha programu za kilimo pekee akisema Chuo hicho mbali na program za kilimo kinatoa programu ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja na sera ya uchumi wa bluu inayompa nafasi ya kuajiriwa kwenye sekta mbalimbali nchini.

“Wengi mnadhani kuwa SUA tunafundisha programu za kilimo tu lakini niwaambie kuwa kuna programu ambazo tunafundisha zina mahusiano na uchumi wa bluu kwani uchumi huo unakamilishwa na programu kama Sayansi ya Mazingira na Usimamizi na nyinginezo”, amesema Bi, Zahra.

Bi. Zahra amezitaja programu ambazo zinafundishwa SUA zenye mahusiano na uchumi wa bluu kuwa ni Shahada ya Sayansi ya Viumbe Hai, Shahada ya Sayansi ya Misitu, Shahada ya Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyapori, Shahada ya Sayansi ya Mazingira na Usimamizi, Shahada ya Sayansi ya Uzalishaji wa Viumbe Maji na Shahada ya Sayansi na Teknoljia ya Chakula.

Kwa upande wake Omari Tunga, Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari upande wa Udahili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amewasihi wanafunzi hao kuanza kujiandaa kujiunga na SUA kwani idadi ya udahili kuanzia mwaka huu unakusudia kuongezeka kufikia wadahiliwa zaidi ya 8,000.

Suhaylla Hamis Juma mwanafunzi mhitimu wa SUA katika Programu ya Elimu ya Viumbe Hai wa Majini na mwajiriwa katika Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Bluu akiongea na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko amesema kupitia uzoefu ambao ameupata kazini amebaini kwamba mbali na programu ambayo amesoma kuna programu nyingine zinazofundishwa SUA ambazo zina mahusiano na Wizara hiyo na inaendana na sera ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia baadhi ya wafanyakazi wanaoshiriki Maonesho ya Elimu ya Juu kinaendelea na mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali za sekondari zilizopo hapa Zanzibar kwa lengo la kukitambulisha Chuo hicho pamoja na kueleza programu zinazofundishwa Chuoni hapo.

Post a Comment

0 Comments