Na: Farida Mkongwe
Wakazi wa mkoa wa Morogoro na maeneo ya jirani wanaofika kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki wametakiwa kufika kwenye banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupata elimu na ushauri wa kitaalamu bure wa kuweza kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanatokana na ulaji wa chakula usiozingatia lishe.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 5, 2023 na Msaidizi wa Wanataaluma Malogo Mkanwa kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Kaya na Mlaji iliyopo Ndaki ya Kilimo SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro.
Bw. Mkanwa amesema katika Maonesho hayo, Idara yao imeleta Wataalamu mbalimbali wanaohusiana na lishe ambao watasaidia kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe ili kuwe na uwiano sahihi kati ya urefu, uzito na kiwango cha mafuta kinachohitajika mwilini mwa binadamu.
“Sasa hivi kuna tatizo la udumavu na utapiamlo ambalo linawakumba watu wengi, tatizo hili alihitaji kwenda hospitali mtu kufanyiwa matibabu ni ushauri tu mtu anatakiwa apewe utaratibu wa ulaji bora hasa kwa kuzingatia yale makundi matano muhimu ya vyakula”, amesema Bw. Mkanwa.
“Hapa kikubwa ambacho tunafanya ni kutoa huduma bure kabisa tunapima watu uzito, urefu tunawapima na kiwango cha mafuta mwilini na baadae tunaangalia uwiano wa hivyo vipimo vitatu nilivyovitaja, baada ya hapo tunampa ushauri kama amezidi au amepungua au yupo sawa tunamshauri namna ya ulaji wake unavyotakiwa na aina ya vyakula anavyotakiwa kula”, amesisitiza Msaidizi huyo wa Wanataaluma.
Maonesho hayo ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yalianza Agosti 1, 2023 ambapo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinashiriki kikamilifu kwa kutoa elimu na kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na Chuo hicho.
0 Comments