SUAMEDIA

Dirisha la Pili la Udahili SUA kufunguliwa Agosti 28, 2023

 Na, Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kinawafahamisha wale wote ambao hawakufanya Udahili kwa awamu ya kwanza ya Udahili au kukosa nafasi ya kuchaguliwa kwenye awamu hiyo ya kwanza katika Chuo hicho kuwa dirisha la Pili la Udahili litafunguliwa Agosti 28, 2023.



Amebainisha hayo Afisa Udahili wa Chuo hicho Bi. Grace Kihombo Agosti 7, 2023 wakati akizungumza na SUAMEDIA katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki mjini Morogoro ambapo amesema wanaotaka kwenda kudahiliwa SUA dirisha tayari limeshafungwa na kwamba wanatakiwa kusubiri Udahili wa pili ambao uko karibuni kufunguliwa.

Amesema kile wanachokifanya kwa sasa katika Maonesho hayo ni kutoa Elimu kwa wale ambao tayari wamekwishatuma maombi yao kuwa Agosti 25, 2023  wanatakiwa kutembelea kwenye akaunti zao ili kuweza kujua amechaguliwa kozi gani katika Chuo chao lakini kwa wale ambao watakuwa wamekosa wanakaribishwa kuomba dirisha la Pili ambalo litafunguliwa Agosti 28 na kumalizika Septemba 3, 2023.

“Kimsingi hapa tunatoa Elimu mbalimbali zinazohusiana na kozi zetu tunazozitoa SUA, wazazi wengi na wanafunzi walipotembelea Banda letu wamepata kunufaika kujua kozi mbalimbali ambazo zinatolewa SUA na  bado watu wanaendelea kuja”, amesema Grace Kihombo

Aidha amewataka wazazi na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo mbalimbali kuelewa kuwa pamoja na kozi za kilimo, SUA pia kuna kozi za Uchumi na Biashara, Ualimu hasa wa masomo ya Sayansi, Sanaa, Misitu, Wanyamapori na Utalii na nyinginezo za Sayansi.

Maonesho hayo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki inayoundwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na wenyeji Morogoro kwa mwaka huu 2023 yamebeba kauli mbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.




Post a Comment

0 Comments