SUAMEDIA

Wananchi wa Madaba waipa SUA ardhi kwaajili ya kujenga Kiwanda cha kuongeza thamani mazao ya misitu ili kuchochea maendeleo.

 Na: Calvin Gwabara – Madaba.

Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo kimekamilisha zoezi la kuwalipa fidia Wananchi 7 wenye shamba la ukubwa wa ekari 151.16 waliokubali eneo lao kutumiwa na Chuo hicho kwaajili ya kujenga Kiwanda cha kuchakata mbao na kuongeza thamani mazao ya misitu katika kijiji cha Magingo wilayani Madaba Mkoa wa Ruvuma.

Viongozi wa SUA wakiongozwa na Prof. Maulid Mwatawala wakizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri Bwana Sajidu Idrisa

Akikabidhi nyaraka na viambatanisho vya malipo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo bwana Sajidu Idrisa, Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii kutoka SUA Dkt. Agnes Sirima amesema makabidhiano hayo yanafanyika mara baada ya kila mwananchi kupatiwa fidia kama ilivyoelekezwa kwa mthamini na kuridhiwa na pande zote mbili.

‘’Baada ya Kitengo cha tathimini cha Mkoa kukamilisha tathimini ambayo iliridhiwa na Wananchi hao saba menejimenti ya Chuo imekamilisha hatua zote za ulipaji wa fidia ya shilingi milioni 54.6 ambayo ilihusisha ardhi pamoja na mazao mbalimbali ambayo yamo kwenye shamba hilo kulingana na sheria na taratibu‘’alieleza Dkt. Sirima.

Aidha amesema kuwa lengo kubwa la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kununua Shamba hilo ni kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata mazao ya misitu hususani mbao na kuziongeza thamani kwa kutengeneza vitu mbalimbali hasa kutoka kwenye msitu wake wa mafunzo wa Ifinga na misitu inayozunguka eneo hilo.

Dkt. Sirima amesema kujengwa kwa kiwanda hicho kutatoa nafasi ya Wanafunzi wa Chuo hicho kupata eneo bora la kujifunza kwa vitendo kama falsafa ya Chuo hicho lakini pia itakuwa sehemu nzuri kwa jamii iishio Nyanda za juu kusini kujifunza mbinu bora na za kisasa za kuongeza thamani ya mazao ya misitu wanayopanda ili kupata faida kubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Bwana Sajidu Idrisa amewaomba SUA kuanza mchakato wa kuanzisha kiwanda hicho ili kiweze kusaidia kuongeza thamani mazao ya misitu ya Wananchi wa Madaba na hivyo kuchangia kuongeza pato la wakulima wa miti na Wilaya.

‘’Kwa niaba ya wananchi wa Madaba niwakaribishe sana kwenye Wilaya yetu, tunaamini ujio wenu utachochea wananchi kulima miti kwakuwa wataona faida baada ya mazao yao kuongezwa thamani maana kwa sasa wanaochakata ni wachache na uzuri wenu mnazo teknoloia nzuri kwa kazi hiyo‘’ alieleza bwana Idirisa.

Amewahakikishia SUA ushirikiano ili waweze kutimiza adhama hiyo ambayo itachochea maendeleo ya hamlashauri na pia akatumia nafasi hiyo kuwakaribisha wadau wengine kuwekeza kwenye halmashauri yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mdaba Bwana Sajidu Idrisa akisisitiza jambo kwa Viongozi wa SUA.

Naibu Makamu kuu wa Chuo Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akitoa salamu za SUA.

Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima (kulia) na Mwanasheria wa SUA Bwana George Zambetakis

Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima akifafana jambo mbele ya Mkurugenzi.

Viongzi wa SUA wakiongozwa na Prof. Maulid Mwatawala wakimsikiliza Mkurugenzi wa Wilaya (hayupo pichani)


Post a Comment

0 Comments