Na: Calvin Gwabara – Ruvuma.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kimesaini Mkataba rasmi na Halmashauri ya Wilaya ya Mdaba Mkoani Ruvuma wa
umiliki wa Shamba la Hekta 10,000 kwaajili ya kilimo cha miti na mafunzo kwa
vitendo kwa wanafunzi wake na jamii.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akitoa salamu za SUA kabla ya kusaini Mkataba huo. |
Akizungumza kabla ya kusaini Mkataba
huo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa
Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la shamba hilo ni kwa
ajili ya mafunzo pamoja na kuongeza mapato.
‘’Hivi Sasa Serikali inahimiza
vyuo kuongeza mapato yake ya ndani ili viweze kujiendesha badala ya kutegemea
ruzuku ya serikali na sisi kama Chuo Kikuu cha Sokoine tumebobea kwenye masula
ya misitu na kupitia uzoefu wetu tulioupata kwenye Msitu wetu wa Olmotonyi kule
Arusha tumeona tuje kuwekeza hapa Madaba na tunaamini tutakuwa mfano kwa vyuo
vingine‘’ alieleza Prof. Mwatawala.
Amesema kuwa kasi ya upandaji wa
miti kwenye shamba hilo la Ifinga imeongezwa nguvu sasa na Mradi wa HEET ambao
umetenga fedha kwajili ya kupanua shamba hilo na kuongeza idadi ya miti
itakayopandwa ambapo kwa mwaka huu pekee wanatarajia kupanda hekta 500.
Prof. Mwatawala amesema eneo la
shamba walilolichukua baada ya kulipa fidia wananchi kwenye kijiji cha Magingo
kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata mazao hayo ya mistu na kuongeza thamani
kutaleta maana endapo kiwanda hicho kitapata miti ya kuchakata hasa kutoka kwenye
shama hilo.
Akitoa salamu za Wilaya ya Madaba
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo bwana Sajidu Idrisa amesema anaamini ujio wa
SUA sio tu kwamba utasaidia kuchochea kasi ya upandji wa miti lakini pia
utasidia kuongeza kipato kwa wananchi watakaoajiriwa kwenye shamba hilo lakini
pia vijiji na Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo bwana Sajidu Idrisa akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo. |
‘’Ili Halmashauri ifanye vizuri
na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo lazima iweze kuwa na mapato ya
kutosha kupitia shughuli zake mbalimbali kwahiyo ujio wenu tunaamini Chuo
kitapata fedha na kuongeza mapato yake ya ndani lakini pia Halmashauri yetu pia
itapata mapato kutoka kwenu na wawekezaji wengine‘’ Alieleza Bwana Idrisa.
Ametumia nafasi hiyo kuwashauri
SUA kuendelea kuongeza kasi ya upandaji wa miti kwenye shamba hilo na kusaidia
kufundisha jamii mbinu bora za kilimo cha miti na namna ya kukabiliana na
majanga ya moto ambayo yanathiri sana kilimo hicho.
Nae Rasi wa Ndaki ya Misitu
Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima amesema tayari wameshapanda takribani
hekta 1000 za miti ya mbao toka mwaka 2018 walipopata eneo hilo na kasi ya
upandaji inaongezeka kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
‘’Tumeendelea kuwa na mahusiano
mazuri na Halmashauri lakini pia wananchi wa kijiji cha Ifinga ambapo katika
kipindi hicho Chuo kimefanya mambo mbalimbali kama mchango wake kwa jamii ikiwemo
ujenzi wa Matundu 20 ya vyoo kwenye
shule ya msingi Ifinga, Kutoa elimu ya moto kwa jamii pamoja na kuwajengea
uwezo viongozi wa kijiji na madiwani‘’ alieleza Dkt. Sirima.
Ameongeza kuwa pamoja na mchango
huo lakini pia Shamba hilo linatoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 ambao hufanya
kazi mbalimbali za upandaji na huduma zingine za shamba na hivyo kujipatia
kipato cha kuendesha familia zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Madaba Mhe. Teofawe Mlewa ambaye ameongoza utiaji saini huo kwa
niaba ya wananchi amesema kuna mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika kata ya
Matumbi baada ya kukaribisha wawekezaji tofauti na hapo awali miaka 7
iliyopita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Mhe. Teofawe Mlewa akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Kijiji cha Ifinga. |
‘’Tuna kila sababu za kuwashukuru wawekezaji na uongozi wa Halmashauri ya Madaba kwa kazi kubwa inayofanywa ya kuleta maendeleo kwenye kata ya Matumbi na kijiji cha Ifinga maana sasa toka Dunia iumbwe kuna mabasi aina ya coaster zinafika hadi kijijini kwakuwa barabara ni nzuri lakini zamani tulikuwa tunatembea kwa miguu kilometa zaidi ya 50 nikiwa mtendaji‘’ alieleza Mhe. Mlewa.
Amewataka viongozi wa vijiji na
kata pamoja na wanachi kuendelea kuwapokea wawekezaji kwenye vijiji vyao kwa
kufuata sheria na taratibu ili kuchochea maendeleo badala ya wao kuwa vikwazo
na kukwamisha uwekezaji kwenye maeneo yao na kurudisha nyuma maendeleo yao.
Mkataba huo kati ya SUA na
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba umesainiwa na kushushuhudiwa na viongozi wa
Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Teofawe Mlewa, Diwani wa kata hiyo
Mhe. Valentine Mtemahuty, Mwenyekiti wa kijiji cha Ifinga Rhomanusi Hangowi na
mtendji wake Baraka Jailos.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZOEZI LA UWEKAJI SAINI MKATABA.
0 Comments