Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimekuwa Chuo cha Kwanza Tanzania kutengeneza teknolojia za kisasa za
kilimo ambazo zinapunguza gharama za uzalishaji wa mazao na hivyo kufanya
kilimo kiwe chenye tija nchini.
Kauli hiyo imetolewa Julai 22, 2023 na Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Kilimo iliyopo Shule ya Uhandisi na Teknolojia SUA Mhandisi Donat Thomas Shukuru wakati akizungumzia teknolojia mpya zinazolishwa na Chuo hicho katika Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam.
Mhandisi Donat amesema Chuo cha
SUA kimejikita katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo zinalenga kufanya kilimo
kuwa na tija na ndio sababu wamekuja na teknolojia ya roboti inalojiendesha yenyewe
inayotumika kwenye uwekaji wa mbolea pamoja na upigaji dawa za kuua magugu na
wadudu shambani.
“Hii teknolojia tunasema
inaleta tija kwa sababu inamsaidia mkulima aweze kupiga dawa au kuweka mbolea
sehemu inayohusika tu yaani sehemu yenye matatizo na hivyo inapunguza gharama
za uzalishaji”, amesema Mhandisi Donat.
Teknolojia nyingine ni
teknolojia za simu ambazo zimegunduliwa na wanafunzi pamoja na Wasimamizi wa Maabara
ya Shule ya Uhandisi na Teknolojia ikiwemo Programu ya Mwagilia ambayo ni ya
kwanza kabisa Tanzania inayotumia taarifa kutoka kwenye satellite kutoa ushauri
wa kiasi cha maji kinachohitajika kumwagiliwa shambani, na kinatoa makadirio ya
kiasi cha maji kinachohitajika kila siku kwa wiki nzima.
Amezitaja Teknolojia nyingine kuwa
ni Programu ya kubaini mimea pamoja na matatizo ambayo yapo kwenye mimea hivyo
kumsaidia mkulima kutambua matatizo ya mmea na kumpa njia ya kutatua matatizo
hayo.
“Tuna Program nyingi, nyingine
ni ile ya simu inayoitwa Smart TB ambayo inawasaidia madaktari pamoja na
wagonjwa wa TB kwa kuweka kumbukumbu za wagonjwa na kuwakumbusha muda wa kunywa
dawa ambapo kwa upande wa madaktari inawasaidia kujua mgonjwa amebakiza muda
gani ili arudi hospitali kiasi kwamba akisahau madaktari wanaweza kumuita
mgonjwa ili aweze kupata matibabu”, amesema Mhandisi huyo.
Mhandisi Donat Thomas Shukuru akitoa maelekezo ya matumizi ya teknoliojia za kisasa kwa mwandishi wa habari Farida mkongwe kutoka SUAMEDIA. Picha na Asifiwe Mbembela. |
0 Comments