SUAMEDIA

SUA yatumia kinga ya ngamia kutibu magonjwa ya binadamu, wanyama, mimea

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Kituo cha Kusini mwa Afrika cha Uchunguzi wa Magonjwa Yanayoambukiza (SACIDS) kimefanikiwa kutumia kinga ya ngamia kwa ajili ya kutengeneza vifaa tiba, chanjo na dawa za kutibu magonjwa mbalimbali yanayowapata binadamu, wanyama na mimea.



Mhadhiri wa SUA wa Idara ya Fiziolojia, Biokemia na Famakolojia ambaye ni Mtafiti kutoka SACIDS Dkt. Edson Kinimi akizungumzia kuhusu kinga ya ngamia. Picha na Asifiwe Mbembela.

Hayo yamebainishwa na Mhadhiri wa SUA wa Idara ya Fiziolojia, Biokemia na Famakolojia ambaye ni Mtafiti kutoka SACIDS Dkt. Edson Kinimi wakati akizungumza na SUAMEDIA jijini Dar Es Salaam ambapo amesema  teknolojia hiyo ya kutumia kinga ya ngamia ni nzuri kwa sababu inatumia gharama ndogo na hivyo kutoa ahueni kwa jamii ya Afrika kwa kuwa nchi nyingi ni zile zinazoendelea.

“Na hii teknolojia sasa tunataka tuanze kuifundisha kwenye Vyuo vikuu vyetu kwa ajili ya kutumia ngamia kutengeneza hizo kinga zenye uwezo wa kuua vijidudu vya magonjwa ndani ya miili ya wanyama na binadamu, hizi kinga za ngamia zinaweza kutumika kutengeneza hata dawa za kuzuia kansa”, amesema Mhadhiri huyo.

“Mojawapo ya kinga ya ngamia ambayo imeshatengenezwa kule Ulaya imeweza kusaidia kuzuia magonjwa ya kuganda kwa damu kwa binadamu,  sasa sisi kama kituo cha Umahiri cha Utafiti, SACIDS ambacho kipo chini ya SUA tumejikita kutumia  kinga hii ya ngamia kutengeneza vifaa vya kutambua magonjwa kwenye jamii kwa haraka sana”, amesema Dkt. Kinimi.

Amesema hadi sasa kwa Tanzania wamezalisha kinga za ngamia tisa zenye uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo na  kinga hizi sasa zinaweza kutumika kwenye magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea.

“Kwa sasa tunazo kinga tisa ambazo zimeonesha uwezo mkubwa wa kutambua virusi vya sotoka ya mbuzi na kondoo na huu ni mwanzo mzuri wa kuendeleza hii kinga katika nyanja nyingine za maradhi hata sumu kwa mfano mtu anaweza kuwa ameng’atwa na nyoka tunaweza kutengeneza vipande vya kinga ya ngamia vya kuzuia ile sumu ya nyoka isimdhuru binadamu”, amesema Dkt. Kinimi.


Post a Comment

0 Comments