SUAMEDIA

Jamii yatakiwa kutumia mbadala wa miti inayokaribia kutoweka nchini

 Na: Farida Mkongwe

Jamiii imetakiwa kutumia miti ya mbao ambayo  haijapewa kipaumbele katika matumizi na kuacha kutumia miti inayokaribia kutoweka ili kuinusu miti hiyo iendelee kuwepo nchini kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.


Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii SUA Mbonea Mweta akizungumzia umuhimu wa miti mbadala. Picha na Asifiwe Mbembela.

Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mbonea Mweta ameiambia SUAMEDIA jijini Dar Es Salaam kuwa kwa sasa badala ya wananchi kutumia miti kama Mvule, Mninga au Mpingo ambayo inatumia muda mrefu kuanzia miaka 70 na kuendelea hadi kuvunwa wanaweza kutumia miti mbadala iliyofanyiwa utafiti na kuonekana ina ubora sawa katika matumizi yao.

Idara yetu ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu tumefanya utafiti na kuja na miti mingine mbadala wa miti hiyo mfano hapo zamani tumezoea kwamba ili mtu atengeneze kinyago ni lazima atumie mpingo lakini baada ya utafiti tumebaini wananchi wanaweza kutumia mti wa Tamarindus Indica (Mkwaju) ambao unapatikana katika mazingira yetu katika utengenezaji wa vinywago, amesema Mbonea.

Akizungumzia miti ya mbao Mbonea amesema Idara yao imeendelea kufanya tafiti zinazohusu matumizi sahihi ya mbao kwa kuoanisha na sifa zake kwa lengo la kutunza rasilimali za misitu nchini na kwamba miti ambayo ina thamani kubwa iwekewe matumizi ambayo yanaendana na thamani yake.

Aidha Mkufunzi huyo amewataka wananchi kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti ili kuleta mabadiliko chanya katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Wananchi tunawahimiza upandaji wa miti, kuzuia ukataji miti ovyo lakini vile vile kutunza rasilimali za misitu ambazo tunazo Tanzania kwa sababu moja ya madhara ya kutokuzuiliwa au kutokupunguzwa kwa hewa ukaa katika mazingira yetu ni uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaleta matatizo mbalimbali hapa nchini, amesema Mbonea.


Post a Comment

0 Comments