SUAMEDIA

Ubalozi wa Japani nchini Tanzania umekabidhi Vitabu 61 kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA

Na Winfrida Nicolaus

Ubalozi wa Japani nchini Tanzania umekabidhi  Vitabu 61 (Sitini na moja) vyenye lugha ya Kingereza  kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA lengo likiwa ni kuwasaidia Watafiti, Wasomi na Wanafunzi  kukuza uelewa katika kuchangia maendeleo ya Rasilimali watu.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda(kulia) akipokea vitabu kutoka kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa ili kuwasaidia Watafiti, Wasomi na Wanafunzi  kukuza uelewa katika kuchangia maendeleo ya Rasilimali watu katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro, jana.

                     

Akikabidhi vitabu hivyo Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa mapema tarehe 27/07/2023  amekabidhi vitabu hivyo kwa Menejimenti ya SUA katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro na kusema kuwa vitabu hivyo  vinahusisha mada mbalimbali ikiwemo Kilimo na Teknolojia, Siasa, Uchumi, Jamii na Utamaduni wa Japani.

Aidha Mhe: Balozi Misawa amesema Japan inaamini SUA ni moja ya Vyuo Vikuu vya matumaini nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wao wa muda mrefu hivyo kupitia vitabu hivyo wataendelea kupata wanafunzi kutoka chuoni hapo vilevile nchi yao inaweza kushirikiana vema na SUA hasa katika Sekta ya Kilimo, Usindikaji wa vyakula kama moja ya sehemu ya kilimo ambayo hata wao wamekuwa wakifanya.

‘‘Tumetoa Vitabu kwa Taasisi zaidi ya 1100 kote ulimwenguni kwa Tanzania Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni Chuo Kikuu cha nne kupatiwa vitabu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma (UDOM) nikiwa kama shahidi Ubalozi wa Japani nchini Tanzania tuliamua kupendekeza SUA kama mwenyeji kwasababu ya ushirikiano wa karibu na wa muda mrefu tulionao baina yetu’’ amesema Mhe. Yasushi Misawa.

Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa Ziara ya Balozi huyo wa Japani SUA ni katika kuendeleza mashirikiano baina yao ambayo yamekuwepo tangu miaka ya 70 na yamekuwa yakiendelea kuimarika siku hadi siku ambapo Japani imekuwa mfadhili katika Miradi mbalimbali chuoni hapo.

Aidha Prof. Chibunda amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi ya Tanzania na nchi za kigeni na kusema kuwa  Japan imekuwa ikikipatia SUA nafasi kwa Watafiti na Wanataaluma wao kufanya kazi pamoja na Watafiti na Wanataaluma wa Kijapani, kuwasomesha ambapo  hivi karibuni kutakuwa na wanataaluma watatu watakaoenda kuanza masomo yao ya Uzamivu katika vyuo mbalimbali nchini Japan.

Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo amesema kukabidhiwa vitabu hivyo na Ubalozi wa Japani ni safari ambayo inakamilisha ushirikiano wa muda mrefu baina ya SUA na nchi hiyo hasa upande wa Tafiti ambapo kwasasa wana Miradi zaidi ya sita ambayo wameshirikiana .

‘‘Katika ushirikiano huo kuna maeneo makubwa ambayo tumesababisha matokeo makubwa ikiwemo Nyanda za Juu Kusini Mbinga ambapo tulianzisha Kilimo kwenye Milima ya Matengo ambapo SUA ilikuwepo kwa muda mrefu na kusaidia katika kuzuia mmomonyoko wa Ardhi lakini pia kwa Morogoro Mradi mkubwa ulioleta matokeo makubwa ni Kilimo cha zao la Vanila na ubora wa zao hilo ni kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanasayansi wa Japani’’, amesema Prof. Karimuribo.

Akielezea umuhimu wa vitabu hivyo kupokelewa chuoni hapo Kaimu Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo SUA Prof. Wulystan Mtega  amesema vitabu walivyokabidhiwa kwa kiasi kikubwa vinahusu Japani lakini katika fani tofautitofauti ikiwemo Kilimo, Siasa, Uchumi na Teknolojia ambapo watumiaji wao wa Maktaba wanahitaji machapisho mbalimbali kama hayo hivyo vitawasaidia katika kuelewa mbinu mbalimbali ambazo Japan wamekuwa wakizitumia katika kujikwamua kiuchumi.                                                                                                                              

 

Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa akizungumza mara baada ya kukabidhi vitabu 61 kwa Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro, jana.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda akizungumza na kumkaribisha Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa alipowasili Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), jana.

Kaimu Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo SUA Prof. Wulystan Mtega akishukuru Ubalozi wa Japan kwa kuwaletea vitabu mara baada ya Menejiment ya SUA kupokea vitabu 61 katika Hafla iliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro, jana.

Naibu Makam Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof . Maulid Mwatawala akitoa Historia fupi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mara baada ya Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa kuwasili chuoni hapo kwa shughuli ya makabidhiano ya vitabu toka Ubalozi wa Japan Tanzania. Jana.

Baadhi ya wafanyakazi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakishuhudia makabidhiano ya vitabu kutoka Ubalozi wa Japan Tanzania katika Hafla iliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro, jana.



Katika Picha ya pamoja Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa (wa kwanza kushoto waliokaa), Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda (katikati waliokaa), Menejimenti ya SUA na wafanyakazi wa SUA mara baada ya makabidhiano ya vitabu kutoka Ubalozi wa Japan Tanzania, jana.

                             

 KATIKA VIDEO BOFYA HAPA CHINI

Post a Comment

0 Comments