Na Adam Maruma
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mh. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba amesifu kazi nzuri inayofanywa na SUA katika kutoa elimu kwa wataalam mbalimbali wa kilimo ambao wamekuwa kichocheo katika kuinua Sekta ya kilimo nchini.
Amebainisha hayo nyumbani kwake jiji Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa SUA kwenye sekta ya kilimo
Mh. Warioba amesema kuwa wakati Tanzania inapata uhuru wataalam katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo walikuwa wachache sana hata hivyo jitihada mbalimbali zilianzishwa na serikali ili kupata wataalam katika sekta hizo na hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzishwa na baadae Chuo cha Kilimo Morogoro kikiwa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo miaka michache baadae kikawa Chuo Kikuu kamili kinachotoa wataalam wa kilimo.
‘’ Kilimo ni uti wa mgongo wa nchi hii na kwa wakati huo tulikitegemea sana nadhani tulipopata uhuru tulikua na wataalam wachache, kwa mafano nyanja zingine kama uhandisi walikua wawili tu, na madaktari walikua wachache sana, na kwa kilimo kulikua na maafisa ugani kwa ngazi za chini hivyo ilionekana kuna umuhimu wao tukaona tuanzishe mafunzo ya juu kwa upande wa kilimo na hapo ndipo baadhi ya vitengo vilivyoanzishwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mojawapo kilikuwa ni kitengo cha Kilimo’’, amesema Mh. Warioba.
Aidha Mh. Warioba amesema kuwa kutokana na umuhimu mkubwa wa wataalam wa kilimo Serikali iliamua kuendeleza Idara ya Kilimo kuwa Chuo Kikuu kamili ili ishughulikie eneo la kilimo pekee na hivyo michakato ikaendelea na hatimae ilipofika mwaka 1984 bunge likapitisha sheria ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Morogoro ambapo baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Edward Moringe Sokoine kwa heshima ya Waziri Mkuu huyo kikapewa jina lake la Sokoine.
Amesema kuwa uanzishwaji wa vyuo vikuu nchini ni jitihada za serikali katika kuendeleza elimu kwa kuzalisha wataalam wenye tija kwenye nyanja mbalimbali na kuanzishwa kwa SUA ni moja ya za njia ya kuendeleza wataalam hasa kwenye sekta ya kilimo ambapo kuna maswala mbalimbali yanayohitaji elimu ya kutosha kutoka kwa wataalam waliopo kwenye sekta hiyo ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya shughuli zao kwa tufanisi zaidi.
‘’Kwanza niseme vyuo vikuu unavyoviona hii leo ni sehemu ya jitihada za nchi kuendeleza elimu na SUA ni mojawapo kati ya vyuo hivyo vikuu, ambacho kinatoa elimu ya juu zaidi katika eneo la kilimo na sio kwamba wanafundisha kilimo peke yake bali kuna mambo mengi yanahusiana na kilimo kama vile uhandisi kilimo”, amesema Mkuu huyo wa SUA.
Jaji Warioba ameongeza kuwa nchi ilipopata uhuru kilimo kilikuwa cha chini sana kwa sababu wakulima walikua wanatumia njia za asili kwa vile hawakua na maarifa ya kutosha kuhusu kilimo bora na kuwapelekea kushindwa kutumia njia za kitaalam ili kuweza kulima kwa tija, Serikali kwa kuona umuhimu wa kilimo iliamua kukipa kilimo nafasi ili nchi iweze kujitosheleza kwa chakula na pia kuweza kujipatia fedha za kigeni kwa kuuza mazao nje ya nchi na kukuza uchumi wa nchi.
Hata hivyo amesema kilimo katika kipindi hicho kimekuwa na kauli mbiu nyingi za kuvutia ikiwemo Kilimo ni Uti wa Mgongo, Kilimo ni Siasa , na Chakula Bora Shambani ambapo kauli mbiu hizo ni njia zilizolenga kuwaamsha wananchi kuingia katika kilimo na kukifanya kama kazi hivyo SUA ina mchango mkubwa katika kutoa elimu lengo ni kuendelea kukifanya kilimo kuwa kazi muhimu kwa uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Jaji Warioba ameendelea kusema kuwa SUA imekuwa ikifanya kazi zake kuu tatu ikiwemo kutoa mafunzo kwa nadharia na vitendo pamoja na kufanya tafiti mbalimbali za kilimo ambapo kitaendelea kufanya hivyo na pia kuendelea kutoa ushauri katika maeneo hayo kwa kuwa yanayokwenda kwa pamoja.
Vilevile amesema SUA imekua Chuo Kikuu pekee nchini kinachojikita katika masuala ya kilimo kwa upana wake na katika kipindi hiki ambacho hali ya hewa duniani inabadilika ndio umuhimu wa SUA unapozidi kuongezeka kwa kuwa wameendelea kuhakikisha wakulima nchini wanalima kwenye majira ya aina yoyote ile iwe kiangazi au masika hasa katika kipindi hiki ambapo dunia inakabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Mh. Jaji Warioba ameipongeza SUA kuanzisha mashamba darasa yaliyopo ndani ya Chuo na kusema kuwa mafunzo kwa vitendo yanaonesha mfano wa namna shamba linavyotakiwa kuwa, na pia uwepo wa mabwawa ya Samaki, na karakana ambayo yamekuwa msaada kwa wanafunzi wanaosoma SUA, vilevile amefurahishwa na uwepo wa mpango wa Atamizi kwa vijana na hivyo SUA kuwa mfano wa vitendo na wahitimu wengi watakuwa vizuri kwenye eneo la vitendo.
0 Comments