Na Calvin Gwabara
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimesaini rasmi Mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma
wa umiliki wa Shamba la Hekta 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miti na mafunzo
kwa vitendo kwa wanafunzi wake na jamii.
Viongozi wakiweka saini kwenye mkataba huo |
Akizungumza kabla ya kusaini Mkataba
huo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa
Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu
Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda
amesema lengo la shamba hilo ni kwa ajili ya mafunzo pamoja na kuongeza mapato.
‘’Hivi Sasa Serikali inahimiza
vyuo kuongeza mapato yake ya ndani ili viweze kujiendesha badala ya kutegemea
ruzuku ya Serikali na sisi kama Chuo Kikuu cha Sokoine tumebobea kwenye masuala
ya misitu na kupitia uzoefu wetu tulioupata kwenye Msitu wetu wa Olmotonyi kule
Arusha tumeona tuje kuwekeza hapa Madaba na tunaamini tutakuwa mfano kwa vyuo
vingine‘’ alieleza Prof. Mwatawala.
Amesema kasi ya upandaji wa miti
kwenye shamba hilo la Ifinga imeongezwa nguvu sasa na Mradi wa HEET ambao umetenga
fedha kwa ajili ya kupanua shamba hilo na kuongeza idadi ya miti itakayopandwa ambapo
kwa mwaka huu pekee wanatarajia kupanda hekta 500.
Prof. Mwatawala amesema eneo la
shamba walilolichukua baada ya kulipa fidia wananchi kwenye kijiji cha Magingo
kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata mazao hayo ya misitu na kuongeza thamani
kutaleta maana endapo kiwanda hicho kitapata miti ya kuchakata hasa kutoka
kwenye shama hilo.
Akitoa salamu za Wilaya ya Madaba
Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo Bw. Sajidu Idrisa amesema anaamini ujio wa
SUA sio tu kwamba utasaidia kuchochea kasi ya upandaji wa miti lakini pia utasaidia
kuongeza kipato kwa wananchi watakaoajiriwa kwenye shamba hilo na pia vijiji na
Halmashauri.
‘’Ili Halmashauri ifanye vizuri
na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo lazima iweze kuwa na mapato ya
kutosha kupitia shughuli zake mbalimbali kwa hiyo ujio wenu tunaamini Chuo
kitapata fedha na kuongeza mapato yake ya ndani lakini pia Halmashauri yetu pia
itapata mapato kutoka kwenu na wawekezaji wengine‘’, alieleza Bw. Idrisa.
Ametumia nafasi hiyo kuwashauri
SUA kuendelea kuongeza kasi ya upandaji wa miti kwenye shamba hilo na kusaidia
kufundisha jamii mbinu bora za kilimo cha miti na namna ya kukabiliana na
majanga ya moto ambayo yanaathiri sana kilimo hicho.
Nae Rasi wa Ndaki ya Misitu
Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima amesema tayari wameshapanda takribani
hekta 1,000 za miti ya mbao toka mwaka 2018 walipopata eneo hilo na kasi ya
upandaji inaongezeka kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
‘’Tumeendelea kuwa na mahusiano
mazuri na halmashauri lakini pia wananchi wa kijiji cha Ifinga ambapo katika
kipindi hicho Chuo kimefanya mambo mbalimbali kama mchango wake kwa jamii ikiwemo
ujenzi wa Matundu 20 ya vyoo kwenye
shule ya msingi Ifinga, Kutoa elimu ya moto kwa jamii pamoja na kuwajengea
uwezo viongozi wa kijiji na madiwani‘’, alieleza Dkt. Sirima.
Ameongeza kuwa pamoja na mchango
huo lakini pia Shamba hilo linatoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 ambao hufanya
kazi mbalimbali za upandaji na huduma zingine za shamba na hivyo kujipatia
kipato cha kuendesha familia zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Madaba Teofawe Mlewa ambaye ameongoza utiaji saini huo kwa niaba
ya wananchi amesema kuna mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika kata ya
Matumbi baada ya kukaribisha wawekezaji tofauti na hapo awali miaka 7
iliyopita.
‘’Tuna kila sababu za kuwashukuru
wawekezaji na uongozi wa Halmashauri ya Madaba kwa kazi kubwa inayofanywa ya
kuleta maendeleo kwenye kata ya Matumbi na kijiji cha Ifinga maana sasa toka
Dunia iumbwe kuna mabasi aina ya coaster
zinafika hadi kijijini kwakuwa barabara ni nzuri lakini zamani tulikuwa
tunatembea kwa miguu kilometa zaidi ya 50 nikiwa mtendaji‘’, alieleza Mlewa.
Amewataka viongozi wa vijiji na
kata pamoja na wananchi kuendelea kuwapokea wawekezaji kwenye vijiji vyao kwa
kufuata sheria na taratibu ili kuchochea maendeleo badala ya wao kuwa vikwazo
na kukwamisha uwekezaji kwenye maeneo yao na kurudisha nyuma maendeleo yao.
Mkataba huo kati ya SUA na
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba umesainiwa na kushuhudiwa na viongozi wa
Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Teofawe Mlewa, Diwani wa kata hiyo Mhe.
Valentine Mtemahuty, Mwenyekiti wa kijiji cha Ifinga Rhomanusi Hangowi na Mtendaji
wake Baraka Jailos.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akitoa salaam za SUA kabla ya kusaini Mkataba huo |
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Bw. Sajidu Idrisa akizungumza kabla ya kusaini Mkataba huo |
Picha ya pamoja ya viongozi wa SUA na viongozi Wawakilishi wa wilaya ya Madaba baada ya kusaini Mkataba |
0 Comments