Na: Farida Mkongwe
Hospitali ya Rufaa ya Wanyama iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imekuwa ni msaada mkubwa kwa wanyama wanaougua magonjwa sugu yanayoshindikana kutibiwa katika kliniki mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa Julai 20, 2023 na Prof. Mshiriki kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya Claudius Luziga akiwa kwenye Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu huduma zinazotolewa na hospital hiyo.
Prof. Luziga amesema hospitali
hiyo inatoa huduma za juu zaidi ikiwemo kupiga X-ray ambazo ni zile za digitali ili kujua tatizo alilonalo mnyama,
huduma za kuboresha wanyama ikiwemo uhimilishaji
na huduma kama Utra Sound na upasuaji
mkubwa ambao hauwezi kufanyika katika kliniki ndogo ndogo.
“Wanyama huwa wanakuja Hospital
ya Rufaa au wakati mwingine tunawafuata kule kwenye mazizi pale inapotokea
dharura labda wanyama wanakufa wengi basi wakulima wanatoa taarifa na wataalamu
wetu wanawafuata”, amesema Prof. Luziga.
Amesema kuwa wananchi wakifika
kwenye banda la SUA lililopo ndani ya viwanja hivyo watapata elimu ya kutosha
kuhusu huduma zinazotolewa na Hospital hiyo na kwamba sasa wafugaji hawana
sababu tena ya kuangaika au kuwa na hofu kuhusu matibabu makubwa ya wanyama
wao.
0 Comments