Na: Amina Hezron, Morogoro
Mkuu wa
Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, Mhe. Judith Nguli amekipongeza Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kufanya tafiti za kisayansi zenye kusaidia
kuinua tija katika kilimo na ufugaji nchini.
Mkuu wa
Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli(wa nane kutoka kulia mstali wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa kilimo na Waratibu wa
Mradi (Picha zote na Amina Hezron) |
Mhe. Nguli
ametoa pongezi hizo wakati akifungua warsha iliyokutanisha wadau wa kilimo kwa ajili
ya kutoa mrejesho wa utafiti uliohusu Utayarishaji Shirikishi wa Huduma za Hali
ya Hewa ili Kuboresha Uhakika wa Chakula, Lishe na Afya nchini Tanzania.
Amesema matokeo
hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa wilaya ya Mvomero ni moja kati ya maeneo
yanayopitia changamoto ya Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Hali ya Hewa kwa
ujumla hivyo yatasaidia wananchi kufahamu vyema na kushiriki kikamilifu katika
matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kilimo.
“Ni
ukweli usiopingika sisi Wilaya ya Mvomero ni waathirika wakubwa wa mabadiliko
ya tabianchi na hali ya hewa na yametuathiri sana, ukipita au kutembea katika
maeneo yetu, kata zetu utaona namna gani swala hili lilivyotuathiri lakini
matokeo haya yamekuja kwetu kwa muda muafaka” amesema Mhe. Nguli
Aidha
ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kujipanga zaidi ili kuhakikisha
taarifa za utabiri wa hali ya hewa wanazotoa zinawafikia vizuri na kwa usahihi wananchi
wa hali ya chini ili waweze kupanda kulingana na wakati kulingana na msimu
husika.
Akizungumza
juu ya manufaa waliyopata wananchi kutokana na utekelezwaji wa mradi huo katika
wilaya ya Mvomero na Mlimba Kaimu Mratibu wa Mradi huo kutoka SUA Dkt.
Sylvester Haule amesema kuwa kwa sasa wananchi hao wanafikiwa na taarifa za
utabiri wa hali ya hewa zinazolenga eneo dogo na si eneo kubwa kama ilivyokuwa
hapo awali ambazo kuaminika kwake
kunakuwa kukubwa.
“Kwahiyo
mkulima anaweza akajua kuwa msimu huu labda mvua zitakuwa ni kidogo kwa maana
hiyo basi ataangalia mazao ambayo yanaweza kustahamili hizo mvua kidogo au
labda mvua zitakuwa ni nyingi zitanyesha kwa muda mfupi basi tuyahifadhi maji
hayo au tupande mazao ya muda mrefu pia sio ya muda mfupi” alifafanua Dkt.
Haule.
Amesema
wakulima wananufaika kutokana na uelewa ambao tayari wameshakuwa nao kuhusu
matumizi ya taarifa na huduma za hali ya hewa pia wamehamasika katika
kuzitafuta na kuzifwata taarifa za hali ya hewa na inaleta urahisi kwa
wazalishaji na wachakataji.
Mradi huu wa miaka miwili umekuwa ukitekelezwa kuanzia mwezi Aprili 2021, na kumalizika 2023 kwa ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Taasisi ya Michelsen (CMI) ya nchini Norway, Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Tabianchi na Mazingira (CICERO) ya Norway, kituo cha Utafiti cha Norway (NORCE) Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Taasisi nyinginezo zilizoko Norway.
Wadau wa kilimo wakijadiliana namna sahihi ya kumsaidia mkulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati ya utabiri wa hali ya hewa
Wadau wa kilimo wakijadiliana namna sahihi ya kumsaidia mkulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati ya utabiri wa hali ya hewa |
Wadau wa kilimo wakijadiliana namna sahihi ya kumsaidia mkulima kupata taarifa sahihi na kwa wakati ya utabiri wa hali ya hewa. |
0 Comments