Na: Tatyana Celestine
Makatibu Mahsusi Tanzania wameshauriwa kujiweka mahala wanapostahili Kitaaluma na kuondokanana kutoaminika mahala pa kazi ikiwa ni pamoja na kujiendeleza kielimu, kuwa waadilifu, kuongeza ufanisi na tija,kuwa wawazi pamoja na uwajibikaji.
Hayo yamesemwa na Mwalimu Charles Magaya ambaye ni mtoa mada muwezeshaji katika Mkutano wa 10 wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi Tanzania unaoendelea mjini Zanzibar kwa lengo la kukumbushana wajibu na majukumu ya kazi kupitia mada isemayo Ufanisi wa Utendaji kazi wa Makatibu Mahsusi katika ofisi za umma.
Mwalimu Magaya amesema anaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali Makatibu Mahsusi katika kuwapa stahiki zao kikamilifu mahala pa kazi hivyo nao wahakikishe wanafanya kazi Kitaaluma ili kuonesha umuhimu wao mahala pa kazi.
Aidha Mwalimu Magaya ameongeza kuwa Kuna makundi matatu ya Makatibu Mahsusi na kuyataja makundi hayo kuwa ni wale wanaofanya kazi kikamilifu, wanaofanya kazi wastani na wale ambao wamelegalega hivyo kuyataka makundi mawili ya mwisho yatumie Fursa hiyo kujifunza kupitia wanaofanya vizuri pamoja na kujiendeleza kielimu kwani anategemea mwaka ujao kuona wengi wao watakuwa wamejiendeleza na kujiunga na ngazi ya Shahada ambapo Sasa ni ruksa kwao.
Mkutano wa 10 wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi Tanzania umeanza Mei 23, 2023 na utamalizika Mei 27 , 2023 ukiwa na kauli mbiu isemayo "Nidhamu,Uadilifu,na Utunzaji Siri sehemu za kazi ni Chachu ya Maendeleo Kitaaluma".
0 Comments