Na: Winfrida Nicolaus
Serikali ya Norway
imeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kilimo lakini pia Tafiti
kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda akimkaribisha Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elizabeth Jocobsen (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Hayo yamebainishwa May
18, 2023 Mkoani Morogoro na Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elizabeth
Jocobsen alipofanya ziara yake SUA ambapo amesema chuo hicho kimekuwa Chuo
Kikuu chenye umuhimu mkubwa kwa Tanzania na sehemu zingine kutokana na mafunzo
wanayotoa ambayo si ya kinadharia pekee lakini pia kwa vitendo ambayo yanawasaidia
wanafunzi wao pindi wanapoenda kwenye soko la ajira ama kujiajiri.
Amesema Norway na
SUA wamekuwa na ushirikiano uzuri kwa zaidi ya miaka 5o sasa kwa kuwa ni
Taasisi muhimu kwa ajili ya mafunzo ya Sayansi ikiwemo Ufugaji wa Samaki hivyo
kuna sehemu nyingi ambazo wanaweza kushirikiana na kwa wakati huu si kilimo
pekee ambacho watajikita nacho zaidi lakini pia wanaenda kufanya tafiti kuhusiana
na Hali ya Hewa lengo likiwa ni kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elizabeth Jocobsen (wa pili kulia) akisikiliza maelezo ya mmoja wa vijana waatamiwa katika kituo kilicho chini ya PASS kwa kushirikiana na SUA |
“Nimevutiwa na
shughuli mbalimbali nilizoziona hapa hivyo najisikia fahari kwa uhusiano wetu ambao
umeendelea kujengeka hasa kwa ajili ya Kituo cha Hewa Ukaa (Carbon Monitory
Center) ambapo tunaenda kufanya mazungumzo ili kuona ni namna gani tunaweza
kushirikiana na kuweza kuihusisha SUA na ajenda tuliyonayo kuhusiana na
Mabadiliko ya Tabianchi”, amesema Balozi. Elizabeth
Kwa upande wake
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda
amesema ujio wa Balozi huyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali ya Awamu
ya Sita lakini zaidi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuvitaka vyuo
vikuu nchini kutokuwa vyuo vikuu vya watu wa ndani pekee bali vifanyiwe umataifishaji
‘international’ sio tu kupata wanafunzi kutoka nje ya nchi lakini pia walimu.
“SUA imekuwa
mstari wa mbele kwenye utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kufikia Balozi
mbalimbali, kuwakaribisha vilevile kuwajengea uelewa ili kuja kuona kuwa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo chenye historia kubwa kina mambo gani ambayo
yanafanyika, jinsi gani kinatoa mafunzo kwa wanafunzi wake, tafiti gani zinafanyika
na wakishajua hayo inakuwa rahisi hata kuwaomba mkawa na ushirikiano ambao
utazaa matunda”, amesema Prof. Raphael Chibunda
Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elizabeth Jocobsen akiwa ameshika tunda katika kituo Atamizi |
Ameongeza kuwa Norway sawa na nchi nyingine duniani wanatilia mkazo kwenye mambo ya Mabadiliko ya Tabianchi hivyo waatafanya mazungumzo na kuona kama chuo chao kinaweza kuendelea kutoa utaalam, ushauri kwenye eneo hilo kwa manufaa ya nchi.
Maeneo
aliyotembelea Balozi huyo wa Norway ndani ya SUA ni pamoja na Maabara ya
Sayansi iliyoko Kampasi ya Solomon Mahlangu ambayo ilijengwa chini ya mradi
ambao uligharamiwa na watu wa Norway, Kituo Atamizi kilichopo chini ya PASS ili
kujionea upanuzi wa ajira kwa vijana kwenye Kilimo, Kituo cha Hewa Ukaa
vilevile Uchumi wa Buluu sehemu ambayo inatumika kwa ajili ya tafiti lakini pia
ufugaji wa Samaki na viumbe maji wengine.
Pichani chini Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elizabeth Jocobsen akijionea mambo mbalimbali wakati alipotembelea SUA
0 Comments