SUAMEDIA

Makatibu Muhtasi, Watunza kumbukumbu SUA, washiriki Mkutano Mkuu (TAPSEA) Zanzibar

Na: Tatyana Celestine

 Makatibu Muhtasi pamoja na Watunza kumbukumbu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, wataungana na Makatibu Muhtasi wote nchini mjini Zanzibar katika Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania  (TAPSEA) utakaofanyika kwa siku nne na pia wakitegemea kufanya kiapo cha utendaji wa kazi zao mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kufunga mkutano huo.

Makatibu Muhtasi pamoja na Watunza kumbukumbu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA safarini kuelekea Zanzibar katika mkutano Mkuu wa Mwaka 2023 wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania  (TAPSEA) 

 

Akizungumza na SUAMEDIA baada ya kuwasili mjini Zanzibar  Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Muhtasi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUASECA) Bi. Joyce Josephat Mwiyola  amesema mkutano huo unaofanyika Zanzibar umekuwa maalumu kutokana na wao kukutanishwa kwa pamoja na watunza kumbukumbu ikiwa ni agizo la Rais Samia ambapo kwao imekuwa ni fursa ya kukutana na wengine kubadilishana mawazo katika kazi, na pia kufanya kiapo kwa pamoja tofauti na miaka ya nyuma.

 

 Bi. Mwiyola amesema kuwa zoezi la kiapo lilikuwa halijatiliwa mkazo kipindi cha nyuma na kupelekea kuvuja kwa siri katika maofisi na sasa Rais wa Samia ameweza kuwaunganisha Makatibu Muhtasi pamoja na Watunza kumbukumbu kufanya kiapo ambacho kwao itakuwa ni muhimu kwani itawafanya wajidhatiti katika kazi lakini pia itawasaidia kufanya kazi kwa usiri bila kusababisha matatizo mahala pa kazi.

 

  Aidha amesema kuwa mafunzo yatakayofanywa yatahusianisha na Huduma kwa mteja, Utawala bora, Utunzaji wa Nyaraka na kumbumbu za ofisi, maadili ya kazi pamoja na ustawi katika muonekano wao pamoja na kukumbushwa wajibu na kufanya maboresho katika kazi kwani kukaa bila kupata mafunzo kunapelekea kufanya kazi kwa mazoea hivyo uadilifu kupotea katika maeneo ya kazi.

 

  Nae mshiriki wa mkutano huo kutoka SUA Katibu Muhtasi Bi. Mwanahabu Omari amesema kuwa amekishukuru Chuo kwa kutoa nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kwani wanapata nafasi ya kukutana na watu wengine, kujiimarisha katika utendaji kazi na fursa ya kubadilisha mazingira ambapo watakaporudi kazini watakuwa wapya.

 Mkutano Mkuu wa kumi wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi Tanzania Mwaka 2023 umejumuisha zaidi ya watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi zaidi ya 4000 ambapo SUA peke yake imepeleka idadi ya makatibu muhtasi 37 na watunza kumbukumbu 21 na kufanya jumla yao kuwa 58 ambapo kumekuwa na ongezeko ukilinganisha na mwaka 2022 ambapo idadi ya washiriki katika mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma ilikuwa 48 .

 



Post a Comment

0 Comments