SUAMEDIA

SUA kuazimisha Kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine

Na: Josephine Mallango

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika kuazimisha kumbukizi ya 18 ya Hayati Edward Moringe Sokoine imetoa wito kwa vijana kujifunza kuchukia utegemezi na kutumia fulsa zilizopo hasa katika sekta ya kilimo katika kujipatia  ajira. 

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Makamu Mkuu Chuo (SUA) Prof. Raphael Chibunda, kuhusiana na Maonesho ya Wiki ya Kumbukizi ya Sokoine.


Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa  amesema lengo kuu la kumuenzi Edward Moringe Sokoine ni kukiwezesha Chuo kujitathimini jinsi wanavyotekeleza majukumu ya msingi kwa vitendo katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti ili kupambana na changamoto za sekta ya kilimo sambamba na kutoa ushauri wa kitaalam kwa wadau mbalimbali .

Aidha Prof. Muhairwa amesema kuwa malengo mahususi ni kukitangaza chuo ndani na nje ya nchi , kutoa fulsa kwa wataaluma na watafiti kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali, kuenzi mambo ambayo  Sokoine alisimamia utekelezaji wake  kwa bidii ikiwemo uadilifu, utii wa mamlaka, kufanya kazi kwa bidii na kupiga vita rushwa ya aina zote  sanjari na kusambaza na kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo na ubunifu miongoni mwa wakulima , wafugaji na wavuvi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kumbukizi ya Edward Moringe Sokoine SUA, Prof. Samwel Kabote  amesema  wataalam wanaozalishwa chuoni hapo  siyo tu wanaenda kuwa wanasanyansi tu  bali wanakuwa wataalam wa vitendo kwa kufika katika maeneo mbalimbali hasa ya vijijini katika kutoa elimu  kwa wakulima wadogo na wakubwa na kusambaza tafiti mbalimbali.

Amesema hiyo inatokana na Hayati Sokoine kuwa kiongozi wa pekee aliyefanya kazi kwa vitendo na kuchukia utegemezi jambo ambalo vijana wote wanapaswa kuliiga  katika kutokomeza utegemezi na kutumia  fulsa zilizopo  na ndio mana serikali imekuja   na  mkakati wa Building a Better  Tomorrow  (BBT)   kupitia Wizara ya Kilimo unaolenga kuandaa fulsa za ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo. 

Kwa upande wake Dr. Suzana Samson  Nyanda  kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA , amemuelezea  Hayati  Sokoine alikuwa  kiongozi mchapakazi na mzalendo  anayefuatilia  utekelezaji kwa vitendo  na  kwamba bado kilimo hakijawa na sura nzuri  kwa sasa lakini mikakati inayoendelea inaweza kupelekea vijana kufanya kilimo kwa kuwa hivi sasa vijana  wengi wanakwepa kutokana  na kuhitaji mafanikio ya haraka ambapo katika kilimo kunahitaji  uwekezaji wa muda.

Aidha Maonesho ya Wiki ya Kumbukizi ya Sokoine yamebeba kaulimbiu “Mazingira wezeshi kwa vijana kushiriki katika kilimo sera, miongozo  na utendaji “.  yataanza Mei 23 hadi 26, 2023 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine zamani ikiitwa Kampasi Kuu ambapo watanzania wote  wanakaribishwa kushiriki na kujifunza na kujionea teknolojia mbalimbali na ubunifu, kushiriki midahalo ya kitaifa , kupata huduma za matibabu kwa wanadamu na mifugo  pamoja na michezo mbalimbali ambapo  itakuwa ni  bure.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kumbukizi ya Edward Moringe Sokoine SUA Prof. Samwel Kabote akizungumzia namna SUA inavyoweza kutumia fursa kwa manufaa ya wanafunzi wake chuoni hapo katika kuelekea Wiki ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine.
Dr. Suzana Samson  Nyanda  kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA  akimuelezea  Hayati  Sokoine alivyokuwa  kiongozi mchapakazi na mzalendo  aliyefuatilia  utekelezaji kwa vitendo. 

Katika Video

Post a Comment

0 Comments