SUAMEDIA

Shughuli za kilimo zinatija kwa vijana - Msimamizi wa shamba la Pinda

 

Na Gladness Mphuru

Vijana waatamiwa kutoka katika kituo cha PASS IAC kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wamefanya ziara katika shamba la aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Pinda (Pinda Farm) kwa lengo la kujifunza na kuongeza ujuzi na maarifa yatakayo wasaidia katika kilimo biashara.

Vijana waatamiwa kutoka katika kituo cha PASS IAC wakiangalia uzalishaji wa Zabibu (Picha zote na Ayoub Mwigune)

Vijana hao wamefanya ziara hiyo Aprili 5, 2023 huko Zuzu mkoani Dodoma lilipo shamba hilo lenye ukubwa wa hekari 71, wakiwa wameambatana na viongozi kutoka PASS.

Akizungumza mmoja wa waatamiwa hao Bw. Isack Mbwilo amesema ziara hiyo imemuwezesha kujifunza mambo mengi mbali na aliyoweza kujifunza akiwa kituoni kwao ambayo ni ufugaji wa Samaki, ufugaji wa Nyuki, kilimo cha matunda na amevutiwa sana na ufugaji wa nyuki kutokana na kutokuwa na gharama kubwa.

Kwa upande wake Bi. Debora Elistus, amesema wameweza kujifunza vitu vingi katika shamba hilo na amevutiwa sana na ufugaji wa Samaki kwa sababu mwanzoni mfugaji huyo atawekeza kwa gharama kubwa lakini kadri anavyozidi kufanya shughuli hiyo ndivyo anazidi kupata faida na gharama za uendeshaji zinapungua.

Akizungumza na waatamiwa hao Msimamizi wa shughuli za shamba la Mizengo Pinda Bw. Joseph Mgunja amesema shughuli za kilimo zinatija kwa vijana kwani zinawapatia ujuzi wa uzalishaji wa mali na taknolojia za uongezaji wa thamani kwenye mazao mbalimbali kama vile teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya dripu ya matone, teknolojia ya kitalu nyumba, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ufugaji wa samaki, uzalishaji wa mazao ya bustani na uoteshaji miche hata kwenye eneo dogo la robo hekari na kuendelea. 

Msimamizi wa shughuli za shamba la Mizengo Pinda Bw. Joseph Mgunja (katikati aliyeshika bakuli) akitoa maeelezo ya namna ya kufuga na kulisha samaki kwa vijana waatamiwa

Aidha amesema ni matumaini yake kuwa vijana hao wamejifunza mengi na kwamba kilimo hakifanywi na watu wa kawaida tu bali hata viongozi wakubwa na mfano ni Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda hivyo ametoa wito kwa vijana wote wafike katika shamba hilo ili kujifunza na kuwa na uzalishaji wenye tija.



Vijana waatamiwa wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara yao mkoani Dodoma



Post a Comment

0 Comments