Na:
Gerald Lwomile, Dodoma
Wananchi na viongozi mbalimbali
walio jitokeza kwenye Maonesho ya Ubunifu 2023 katika uwanja wa Jamhuri jijini
Dodoma, wamekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kusaidia kutatua
changamoto mbalimbali katika sekta ya Kilimo kupitia teknologia walizo zigundua
chuoni hapo.
Mnamo Aprili 26, 2023, Mbunge wa Jimbo
la Muleba Kaskazini na Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara Mhe. Charles
Mwijage mara baada ya kutembelea Banda la SUA, amesema wakulima wengi wamekuwa
wakipata changamoto za magonjwa ya mimea na wanyama na kukosekana kwa malisho ya
kutosha kwa wanyama.
Amesema utatuzi wa changamoto
hizo limekuwa siyo jambo rahisi hivyo tafiti zinazofanywa na SUA zinasaidia
katika kuhakikisha wakulima wanajua njia sahihi za kuepuka na kutibu magonjwa
ya mimea na wanyama.
Amesema SUA imekuwa ikienda na
wakati kwani katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuwepo
kwa maeneo machache ya kuchungia, SUA imejikita katika tafiti za malisho na
tayari wafugaji wameanza kunufaika.
Amesema mbali na malisho pia SUA
imejikita katika kutoa aina mbalimbali ya miche bora ya matunda ambayo inazaa ndani ya miaka 3 na
imesambazwa sehemu kubwa ya nchi
Naye Bwana Zakayo Nistan ambaye
ni mfanyabiashara mdogo maarufu kama Machinga jijini Dodoma, aliyefika kujionea
teknolojia zinazo onyeshwa na SUA amesema bunifu za SUA zimeleta maendeleo
makubwa kwa wananchi hasa katika kuimarisha afya ya binadamu, mimea na wanyama.
Bw. Zakayo Nistan akiwa amebeba panya katika banda la SUA, panya hawa ni maalum kwa ajili ya tafiti |
Amesema utafiti na teknolojia ya
kutumia Panya kutambua eneo ambalo lina mabomu ili yateguliwe na kutambua
makohozi yenye vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu yaaani ‘Tuberculosis’(TB)
ugonjwa ambao ni hatari na husababisha vifo.
Wakati huo huo SUA imekuja na
ubunifu wa mfumo wa kidigitali unaoitwa ‘SmartTB’ unaoweza kufuatilia matibabu
ya mgonjwa wa Kifua Kikuu kwa ajili ya kuhudhuria kliniki kwa wakati ili kupata matibabu
na kujua taarifa za maendeleo ya afya. Hatimaye kujiweka kwenye
mazingira mazuri ya kupona kabisa ugonjwa huo.
Bi Joan Jonathan (aliyevaa miwani ) akitoa maelezo ya namna mfumo wa SmartTB unavyofanyakazi, wa pili kulia ni Prof. Lazaro Busagara Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania |
Akizungumza wakati wa maonesho ya
Wiki ya Ubunifu Tanzania 2023, Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Infomatiki na
Teknolojia ya Habari SUA Bi Joan Jonathan amesema mfumo huo pia unaweza
kumjulisha mhudumu wa afya upande wa kifua kikuu kama kuna mgonjwa wa TB alitakiwa
kufika kliniki ili kupata matibabu na hakufika ili aweze kufuatiliwa.
Amesema mfumo huu unaweza kutuma
ujumbe mfupi yaani SMS kwenye namba ya simu ya mgonjwa na mhudumu wa afya
ambapo mgonjwa atapata ujumbe siku moja kabla ya siku aliyopangiwa kuhudhuria
kliniki. Vivyohivyo, mhudumu wa afya atapata ujumbe siku moja baada ya mgonjwa kutofika
kliniki, na hii itasaidia mhudumu huyo kuwasiliana na mgonjwa ili afike kupata
matibabu. Pia, SmartTB itasaidia kupunguza kuenea kwa kifua kikuu sugu na
maambukizi mapya.
Maonesho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania yameingia siku ya 3 na yanatarajiwa kufikia kileleni Aprili 28, 2023 ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo ni ‘Ubunifu kwa Uchumi Shindani’
Picha chini ni matukio mbalimbali katika maonesho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania
0 Comments