Na: Gerald Lwomile, Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa uthubutu wake wa kutumia fedha zake za mapato ya ndani katika kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu (ASDP) Dkt. Salim Nandonde akifunga warsha ya siku moja ya matokeo ya utafiti wa SATTA (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Akifunga warsha ya siku moja Jijini Dodoma, Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) Dkt. Salim Nandonde amesema SUA ni mfano wa kuigwa katika jambo hilo na kuzitaka taasisi zingine za utafiti kuiga mfano huo.
“Kwetu sisi siyo kuwa unapata kiasi gani cha fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo, lakini ni kwa namna gani unatumia cha kwako ndani kufanya kile ambacho kinawezekana na ndicho kinafanya niseme, kwa kweli hili ni jambo kubwa sana kwa hiyo tunatakiwa kuipongeza SUA kwa kutoa fedha zake na kuwawezesha vijana watafiti kufanya tafiti zao, huo ni ushujaa mkubwa” amesema Dkt. Nandonde
Akizungumzia namna Programu hiyo ilivyotekelezwa katika awamu mbili yaani ASDP I na ASDP II amesema, fedha za kuwezesha utekelezaji wa Programu kutoka kwa Wadau wa Maendeleo zinavyopungua mwaka hadi mwaka.
Awali akifungua warsha hiyo iliyokuwa na nia ya kutoa matokeo ya utafiti wa SATTA katika ASDP, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Shahada za Juu, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu, SUA Prof. Esron Karimuribo amesema SUA pamoja na majukumu yake ya kufundisha, utafiti na ushauri wa kitaalamu, kama taasisi ya umma ni lazima itoe majawabu ya matatizo yanayoikabili jamii ya kitanzania.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Shahada za Juu, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu, SUA Prof. Esron Karimuribo akizungumza na wadau wakati wa kufunga warsha ya SATTA |
Prof. Karimuribo amesema katika kuhakikisha SUA inafikia malengo yake wamewekeza katika kufanya tafiti na kujenga uwezo wa watafiti ambapo hadi sasa SUA ina jumla ya wanataalumu 564. Wale wanoweza kufanya kazi ya utafiti yaani wale walio na Shahada ya Udaktari ni 308 ambao ni sawa na asilimia 54.6.Kupitia watafiti hawa, SUA imeendelea kushika nafasi ya kwanza katika utafiti nchini.
Amesema mwaka 2021 SUA ilianzisha Program ya SUARIS ambayo ililenga kujenga uwezo wa kutoa fedha za mapato ya ndani kwa watafiti ili waweze kufanya tafiti na kutoa majawabu. Mwaka 2021 walitenga shilingi milioni 500, mwaka 2022 walitenga bilioni moja na kwa mwaka huu unaoishia Juni, 2023 pia wametenga bilioni moja na hii inaonyesha SUA inavyozidi kupanda katika matumzi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utafiti.
Naye Mkuu wa Idara ya Sera, Mipango na Menejimenti katika Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. David Mhando, amewashuru wadau wote walioshiriki katika utafiti huo wakiongozwa na Dkt. Suzana Nyanda na Emmanuel Malisa kwani ushiriki wao umeleta matokeo yanayoweza kutumiwa katika utekelezaji wa miradi mingine.
Mkuu wa Idara ya Sera, Mipango na Menejimenti katika Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Prof. David Mhando, akisisitiza jambo katika warsha ya SATTA |
Wakizungumzia utafiti huo Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo kutoka wilaya ya Manyoni Bw. Fadhili Chimsalimu amesema baada ya kuwasilishwa kwa matokeo ya utafiti wa SATTA wameona kuna baadhi ya mianya inayopelekea kupungua kwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ASDP na hivyo ni muhimu kuwepo kwa mashirikiano na kufahamu vizuri miradi na mipango mbalimbali ya kuinua kilimo nchini.
Pichani Chini ni wadau mbalimbali walioshiriki katika warsha ya SATTA
0 Comments