Na JOSEPHINE MALLANGO
Takataka katika chombo cha kuhifadhia uchafu zatajwa kuwa chanzo cha moto uliozuka ghafla katika Benki ya Taifa ya Biashara (NMB) Tawi la SUA majira ya saa 4 asubuhi ya tarehe 20/03/2023.
Kufuatia tukio hilo Wananchi wamepongeza Jeshi la Zimamoto pamoja na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kufika kwa wakati katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzima moto na kuimalisha ulinzi katika eneo lote la Benki.
Akizungumza na SUA Media, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Morogoro, Mkaguzi Emanuel Ochieng amesema wamefanikiwa kuzima moto kwa wakati na wafanyakazi wote 18 na wateja waliokuwepo ndani ya benki hiyo wakati moto huo ukizuka wako salama.
Kaimu Kamanda huyo ametaja chanzo cha moto huo ni takataka zilizokuwa zimewekwa kwenye chombo cha kuhifadhia taka cha chuma na hivyo kusababisha joto ambapo hakuna madhara makubwa katika eneo lililokuwa limeweka chombo hicho mara baada ya kuzima moto huo ambao ulikuwa wa daraja la A uliozimwa na mitungi ya kuzimia gesi na siyo maji.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi wa Polisi Alex Mkama ametoa wito kwa zimamoto kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya vifaa vya kuzimia moto kutokana na kufika katika eneo la tukio na kukuta vifaa vyote vya kuzimia moto vipo lakini wafanyakazi wa Benki wakiwa wamekaa tu pembeni bila jitihada zozote za kujaribu kujihami kuzima moto huo .
Hata hivyo SUA Media ilipoongea na Meneja wa Benki ya NMB Tawi la SUA Witness Mwanga amesema tukio hilo la moto lilikuwa tukio la kupima utayari na wamejifunza kuwa tayari alamu zinapolia na kusogea katika eneo salama la makutano na kwamba katika tukio hilo la moto vyombo vya usalama vimeonyesha namna gani viko tayari katika kukabiliana na majanga ya moto kwa kudhibiti majanga moto yanapotokea.
Kwa upande wa shuhuda ambaye ni mteja aliyekuwepo ndani ya benki hiyo Adam Maluma amesema walishangaa kuona moshi mzito ukitokea katika moja ya chumba cha mtoa huduma za kifedha na hivyo kutakiwa kutoka kwa utaratibu na kuwekwa katika eneo salama la makutano huku taratibu zingine za kuzima moto huo zikiendelea .
Nao mashuhuda Wanje Karikasa Shababi na Habibu Juma wamesema wameshangazwa na Jeshi la Polisi na Zimamoto kwa kuwahi kufika katika eneo hilo huku Jeshi la Polisi likiimarisha ulizi wa hali ya juu kwa polisi wenye silaha kutanda eneo lote la benki hiyo sambamba na uwepo wa Kamanda wapolisi mkoa wa Morogoro muda wote katika eneo la tukio .
Wananchi hao wameliomba Jeshi la Zimamoto na Polisi kuwahi katika matukio mengine ya majanga kama walivyowahi katika tukio hilo la benki ili kuwaepusha hasara mbalimbali wanazokutana nazo wananchi katika maeneo mengine yanayopata majanga kwa madai kuwa wanachelewa kufika .
0 Comments