Wanachuo 186 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, wameshiriki mafunzo kwa vitendo yanayohusiana na Utunzaji na Uhifadhi wa Mifumo ya Ikolojia ya Mwambao wa Pwani na Maji Chumvi (Coastal and Marine Ecosystems) katika Pwani ya Tanzania.
Mafunzo hayo yametolewa 13 Machi 2023 kwenye eneo la lango la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam ambapo Afisa Mhifadhi Mkuu Frank Sima kutoka Wakala wa Misitu Nchini (TFS), Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema kuwa kwa kutembelea maeneo ya hifadhi za ukanda wa Pwani na maji chumvi lengo ni kujifunza manufaa, umuhimu na utunzaji wa mikoko ya Mkoa wa Dar-es-Salaam katika wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, na Kigamboni.
Aidha Bw. Sima amebainisha kuwa zao aina ya mikoko lina faida kubwa za kiikolojia kama vile kuwa sehemu ya mazalia na unenepeshaji wa Samaki, kuzuia mmomonyoko wa udongo utokanao na mawimbi ya bahari na upepo.
Faida nyingine ni pamoja na kufyonza hewa ukaa kwa kiwango kikubwa kuliko miti ya aina zingine, utalii wa kiikolojia na ufugaji nyuki ambapo pia Mikoko inachangia katika kuchuja aina mbalimbali za takataka ngumu na kikemikali ili zisiingie baharini Pamoja na umuhimu wake katika kwa shughuli za kibinadamu kama vile kuni, mbao na fito kwa ajili ya ujenzi na matumizi mengine.
Vilevile wanachuo kupitia Mafunzo hayo wamejifunza aina mbalimbali za mikoko zinazopatikana kwa wingi kwenye Ukanda wa Pwani ya Tanzania kama vile Mkaka, Mkandaa, Msinzi, Mchu, Mpira, Msikundazi, Mkomafi Mweupe, Mkandaa dume, na Mseji.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Elimu ya Viumbe Hai (Biosciences) ya SUA, Dkt. Elly Ligate amesema kuwa kuna umuhimu wanachuo hao wakawa mabalozi kwa kuwaelimisha wengine kuhusu umuhimu wa mfumo wa kiikolojia ya mwambao wa Pwani na Maji chumvi katika afya ya mazingira, ikolojia yenyewe, maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii ili kusaidia utunzaji wa mazingira.
“Kwa kipindi kirefu sasa Dunia inashuhudia madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto Duniani, kuongezeka kwa vimelea vya maradhi na milipuko ya magonjwa kwa sababu afya ya mazingira imetoweka” Amesema Dkt Ligate.
Naye Mtaalamu wa Elimu ya Mimea kwa Vitendo Bw. Gaston Mbilinyi, amewaasa wanachuo hao kuzingatia mafunzo yanayotolewa kwa njia ya vitendo kwani wamepata nafasi adimu ya kuona na kutenda.
Aidha Viongozi wawakilishi wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Bw. Simkoko, Bw. Yusuph na Bw. Mwambelo, Bi. Upendo wamekiri kuwa mafunzo kwa vitendo yamewafungua macho na ufahamu kuhusu uhalisia wa mambo waliyosoma kinadharia chuoni.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo hutoa mafunzo kwa vitendo kila mwaka yanayohusisha wanachuo wa mwaka wa kwanza katika Shahada ya Sayansi za Mazingira na Usimamizi wa Mazingira (BSc. Environmental Sciences and Management).
0 Comments