SUAMEDIA

Wilaya ya Mbarali imeahidi kuendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na mradi wa (EFLOWS) - SUA kutunza vyanzo vya maji.

Na: Amina Hezron, Mbeya

Ili kuhakikisha mazingira ya mto Mbarali na Vyanzo vyake vinatunzwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoni Mbeya Mwl. Missana Kwangura ameahidi kuwajengea mfumo wa maji wanajumuiya ya watumia maji wa Mto Mbarali (JUWAMBA) ili kurahisisha utunzaji wa kitalu cha miche rafiki wa maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoni Mbeya Mwl. Missana Kwangura (Kulia) akizungumza Mtafiti Mkuu wa Mradi wa (EFLOWS) Prof. Japhet Kashaigili alipotembelea kialu hicho cha miti rafiki na maji kwenye na Wanajumuiya ya watumia maji wa Mto Mbarali (JUWAMBA).

Ahadi hiyo ameitoa alipokwenda kutembelea sehemu kilipoanzishwa kitalu hicho kupitia Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) akiwa ameambatana na kiongozi wa mradi huo Prof. Japheti Kashaigili kutoka SUA na kukutana na wanajumuiya hao ambao ndio wanaotunza kitalu hicho.

Amesema kuwa kabla mradi huo haujaisha Halmashauri kwa kushirikiana na wenye mradi pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) watajitahidi kuhakikisha mfumo wa maji umeshakamilika ili kuwatua wakina mama waliopo kwenye jumuiya hiyo ndoo kichwani kwakuwa wanafanya shughuri hiyo ya umwagiliaji kwakuchota maji mtoni na kubeba kichwani.

“Tukiweka mfumo wa maji hapa itasaidia kuoteshwa kwa miche mingi zaidi kutokana na urahisi wa upatikanaji wa maji jambo litakalokwenda kusaidia kupatikana kwa kipato kwa Wanajumuiya hawa ambao wanafanya kazi kwa kujitolea endapo watatumia kitalu hiki kuzalisha na miche ya matunda mwaka mzima ”, alisema Mwl Mwal Kwangura .

Aidha Mwl Kwangura ameshukuru Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kwakuanzisha kitalu hicho cha miti kwakuwa jitihada hizo zinawasaidia sana katika kuungana na malengo ya Serikali ya kuhakikisha kila halmashauri inapanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.

Kwa upande wake mkuu wa mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS)

 Prof. Japhet Kashaigili ameishukuru halmashauri kupitia Mkurugenzi kwa nia yake ya kuhakikisha uendelevu wa mradi huo hasa upandaji wa miti kwenye mito na vyanzo vya maji kwa kutunza kitalu hicho ili kupata miche kupitia wanajumuiya hao ambao wamejengewa uwezo.

“Tulikuwa tunajiuliza tunaondoka tutaondokaje na sisi mioyo yetu ingetuuma sana unapoanzisha kitu kama hiki kwa pesa nyingi halafu siku moja unatembea huku unakuta kimekufa, mimi nishukuru sana kwakuwa tunaona taa nzuri na mwanga  wa tunakoelekea tunaamini kuwa kazi hii tuliyoianzisha sasa unakuwa endelevu kwa maslahi mapana ya Wilaya na Taifa.

Aidha Prof. Kashaigili amewataka Wanajumuiya kufanya kazi hiyo kwa bidii kwakuwa tayari wameshapata watu watakaoshirikiana nao katika shughuri hiyo ya utunzaji wa kitalu pindi mradi utakapomalizika na kuahidi kuwapeleka Wanajumuiya wote SUA kupata mafunzo kuhusu uzalishaji wa miche ya matunda ili kuwaongezea kipato kupitia kitalu hicho na kuendelea kutunza mazingira na vyanzi vya maji.

Mradi huu unatekelezwa na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira na unatekelezwa katika dakio la mto Mbarali katika bonde la mto Rufiji kwa ushirikino na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, Jumuiya za watumia maji, TFS, Wilaya ya Mbarali na Wanging’ombe na jamii, kwa ufadhili wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) na kutelezwa kupitia Sekretarieiti ya Azimio la Nairobi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoni Mbeya Mwl. Missana Kwangura akipanda mti rafiki wa maji nje ya Kitalu hicho kama alama ya ushiriki wa halmashauri yake katika kuendeleza kitalu hicho.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Mwl. Missana Kwangura (Kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa (JUWAMBA) bwana Siasa  juu ya ujenzi wa mfumo wa maji na uendelezaji wa kitalu hicho.



Picha ya Pamoja ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Mwl. Missana Kwangura, Mkuu wa Mradi wa (EFLOWS) Prof. Japhet Kashaigili na Wanajumuiya wa (JUWAMBA).



Post a Comment

0 Comments