Na: Amina Hezron – Mbeya.
Ili kuhakikisha kunakuwa na maji ya kutosha kuendesha mitambo ya kufua umeme kwenye bwawa la Mwl. Julius Nyerere (JNHPP) Wananchi waishio Nyanda za Juu kusini ambapo maji yake yanatoka kujaza bwawa hilo wametakiwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu zinazoharibu vyanzo vya maji na mito ili Tanzania inufaike na Mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) akizungumza na Waadishi wa habari kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji na mito.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) alipotembelea Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kwaajili ya kuona na kufahamu maendeleo ya mradi huo ulipofika toka kuanza kwake.
Amewametaka kuacha kufanya shughuri za Kibinadamu ndani ya mita sitini kutoka kwenye mito na vyanzo vya maji ili kutunza uoto wa asili utakaosaidia kupunguza mtiririko wa maji ambayo yamechanganyika na tope kuelekea kwenye mito mingi na mwisho kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere.
“Tutunze vyanzo vyetu kwa kupanda miti ya asili rafiki na maji na baadhi ya nyasi ambazo zinafaa sana kupunguza tope kwenye mitiririko ya maji mtoni, tuwe na usimamizi imara wa vyanzo vya maji kupitia jumuiya za watumia maji (WUA), tuanzishe shughuli rafiki na mazingira na maji kwenye maeneo ya hifadhi za mito kama ufugaji wa nyuki na miti ya matunda ili kujiongezea kipato, pia kuingiza maeneo yote nchini ya hifadhi ya mito kwenye biashara ya hewa ya ukaa, tufuge kwa tija na kuacha kunywesha mifugo kwenye vyanzo na badala yake zijengwe karo za kunyweshea mifugo mbali na vyanzo vya maji na mito”. Alieleza Prof. Kashaigili.
Aliongeza “tufanye kilimo rafiki na mazingira na kilimo hiki ni pamoja na kulima kwa kutumia makinga maji ambapo unalima kwa kukinga mteremko kwa maana ya kupunguza udongo ambao unamung’unyuka mvua inaponyesha na kuelekea kwenye mito na mwisho kwenye bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na pwani ya Bahari ya Hindi”.
Prof. Kashaigili ameeleza kuwa hayo yote ni matokeo ya tafiti zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika na kuendelea kutoa ushahidi wa kisayansi ambao utawezesha kuondoa ama kupunguza changamoto kama hizo ili kuweza kuwa na maji salama ambayo yatawezesha kuendeleza vizuri miradi mikubwa ya kimkakati kama huo wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.
Amesema lengo la mradi huo wa utafiti ni kupunguza athari za shughuli za kibinadamu na kuhimarisha usimamizi endelevu wa mifumo muhimu ya mito kupitia tathimini ya mtiririko wa maji ya mazingira kuelekea ukanda wa pwani na utekelezaji kwa ushirikiano katika ngazi ya kitaifa na kikanda.
Naye Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Ndugu Florence Mahay amesema kuwa inaonekana dhahiri kuwa ili bwawa liweze kujaa ni lazima matumizi ya maji kule juu yaratibiwe kwasababu shughuli yeyote itakayochukua maji kutoka katika mito hiyo hiyo inapunguza mtiririko wa maji yanayotiririka kwenda katika bwawa hilo la Nyerere.
“Bodi itaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali lakini itaendelea kuhakikisha kwamba sheria za matumizi ya maji zinafatwa kwa kuwa tuna mpango wa kuajiri walinzi wa mito ambao watakuwa wanahakikisha anayetumia maji ni yule tu mwenye kibali na kuhakikisha hakuna mtu anayeharibu vyanzo vyetu vya maji”, alisema Mahay.
Mradi huo wa kufua umeme utagharimu Sh. trilioni 6.5, utazalisha Megawati 2,115 zitakazoongeza nguvu katika Megawati 1,500 zinazowashwa na vyanzo mbalimbali vya sasa na litawezesha Tanzania kujitosheleza kwa mahitaji yake ya umeme na kuuzwa nchi jirani sambamba na kupunguza gharama za umeme kwa watanzania.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wanatekeleza mradi wa mfano wa utafiti wa “Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji kwa kuimarisha Tathimini ya Mtiririko wa Maji ya Mazingira na Utekelezaji wa Mpango Mkakati kwa ajili ya Mazingira wenye Lengo la Kulinda Ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi Kutokana na Athari za Shughuli za Kibinadamu, Tanzania” kwa ufadhiliwa na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa kupitia ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP na kutekelezwa kupitia Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.
Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) Mhandisi. Lutengano Mwandambo akizungumza na jopo la Wanahabari,Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na wataalamu kutoka Bonde la Rufiji juu ya maendeleo ya mradi .
Wanahabari, Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na wataalamu kutoka Bonde la Rufiji wakipata maelezo ya kina kuhusu maendeleo ya mradi huo kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa Mradi. |
1Muonekano wa sehemu ya ukuta wa mradi huo wa JNHPP. |
Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Frorance Mahay akizungumza na Wanahabari kuhusu mchango wa Bonde la Rufiji katika kuongeza maji kwenye Bwawa la Mwl. Nyerere. |
0 Comments