Na: Tatyana Celestine
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinaendelea kujivunia ubora wa tafiti na miradi inayosaidia kukuza na kuibua watafiti wachanga ambao wamekuwa na tija katika kutoa mrejesho wa tafiti zao zilizopelekea kuongeza uwezo wa kufanya utafiti kupitia mafunzo ya Shahada ya Uzamivu yaliyotolewa kwa wanataaluma 12 walionufaika na Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU).
Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU) SUA Prof. Antony Sangeda katika siku ya kuhitimisha Semina ya siku tatu inayokamilisha iwepo wa mradi |
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU) SUA Prof. Antony Sangeda wakati akizungumza na SUAMedia katika siku ya kuhitimisha semina ya siku tatu inayokamilisha uwepo wa mradi huo ambao umedumu kwa miaka 12 SUA na kuwa moja chuo kilichonufaika Tanzania.
Prof. Sangeda amesema wanataaluma zaidi ya mia moja kupitia mradi huo wamepata fursa ya kutoa mafunzo kwa wanataaluma wenzao kuelewa mbinu za kisasa za ufundishaji wa wanafunzi, kuandika dodoso za utafiti na namna ya kutumia mtandao kutoa mafunzo ambao ulisaidia kutoa elimu kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa CORONA.
Ameongeza kuwa faida nyingine ni pamoja na kupata muendelezo wa maeneo ya kufanyia tafiti kama vile eneo la uzalishaji na ukuzaji wa samaki eneo la Magadu ambapo kumewekwa mabwawa makubwa sita yaliyojengwa katika awamu ya pili pamoja na vifaa vilivyojengwa ndani ya jengo ili kusaidia uzalishaji wa samaki kwenye eneo hilo.
Pamoja na mambo mengine mradi huo umesaidia kutengeneza mitaala ambayo inaendelea kutumika akiitaja kuwa ni Shaada ya Umahiri ya Kilimo Ikolojia, Shahada ya Uzamivu ya Ufugaji wa Samaki pamoja na Shahada ya Uzamivu ya Kilimo Biashara ikiendelea kutumika katika Idara mbalimbali chuoni hapo.
Akizungumzia kuhusiana na muendelezo wa mradi huo mara baada ya kuisha Prof. Sangade amesema kuwa kwa sasa DANIDA ambao ni wadhamini wameamua kuendelea kuinua vyuo vichanga nchini tofauti na chuo kama SUA kwani tayari ni chuo kikubwa na kimeshika nafasi za juu pamoja na kutangazwa kutoa Mtafiti Bora kulinganisha na vyuo vingine nchini kwa matokeo hayo pia BSU imetoa mchango wake.
Aidha ametoa hamasa kwa watafiti wachanga kuendelea kujifunza kupitia watafiti waliofanikiwa kupitia mradi huo ambapo BSU imewapa fedha na miradi midogo 13 na waliweza kuonesha matokeo chanya yaliyopelekea kuzalisha miradi mikubwa kwa kutumia programu ya SUARIS iliyoanzishwa na chuo ili kuwasaidia watafiti wachanga kufikia malengo yao.
Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU) ambao ni ushirikiano kati ya watafiti wa SUA na Serikali ya Denmark kupitia vyuo vikuu mbalimbali wakiunganishwa na Shirika la DANIDA utafikia tamati Desemba 2023 baada ya kutekelezwa chuoni hapo tangu mwaka 2021.
KATIKA PICHA WATAFITI KUTOKA SUA NA DENMARK WALIPOTEMBELEA MIRADI MBALIMBALI INAYOFYWA NA SUA IKIWEMO SUGECO NA UCHUMI WA BLUE (MAGADU). PICHA NA GERALD LWOMILE.
0 Comments