Na: Tatyana Celestine
Wakati Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Vyuo vingine nchini Tanzania na Dermark ambao ni washirika katika Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU) kuhitimisha mradi wao Serikali na wanufaika wa mradi kutoka SUA wamekiri kupata manufaa makubwa katika nyanja tofauti ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi ya utekelezwaji wa mradi huo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha Mradi wa Ujenzi wa Vyuo Vikuu Imara (BSU) leo 22 Mach, 2023 kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Caroline Nombo, Mkurugenzi Msaidizi Msimamizi Rasilimali watu Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Sayansi, Elimu na Teknolojia Bw. Sebastian Inoshi amesema kuwa mradi huo umewasaidia watanzania hasa watafiti kwa kuwasomesha na kupata Shahada za Uzamivu na Umahiri pamoja na kutengeneza miundombinu inayosaidia kufanya tafiti katika mazao mbalimbali nchini pamoja na ufugaji wa samaki.
Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa watanzania wananufaika kwa ongezeko la wataalam katika nyanja hizo lakini elimu kutolewa kwa wanafunzi ambao wanapata elimu katika vyuo washirika pamoja na kuwasaidia maafisa Ugani wakiwemo Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Akizungumzia namna mradi huo ulivyoweza kunufaisha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama moja wa Vyuo vilivyofikiwa na mradi huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa mradi huo ambao ni ushirikiano kati ya watafiti wa SUA na Serikali ya Denmark kupitia Vyuo Vikuu mbalimbali wakiunganishwa na Shirika la Misaada la Denmark (DANIDA) katika awamu zote tatu ndani ya miaka kumi ya mradi huo chuoni hapo umekuwa ukiwajengea uwezo wanataaluma ili kuwa watafiti wazuri.
Aidha Prof. Chibunda ametaja awamu ya pili ya mradi huo ililenga katika maeneo makubwa matatu ambayo ni Kilimo Mseto, Ufugaji wa Samaki pamoja na uongezwaji thamani kwenye Mazao ya Kilimo na kusema kuwa katika maeneo hayo Chuo kimenufaika zaidi katika upande wa samaki kwa kuwasomesha walimu na kuongeza miundombinu ya ujenzi maeneo ya ufugaji wa samaki chuoni hapo.
Hata hivyo Prof. Chibunda amesema kwa upande wa Kilimo Mseto SUA wamenufaika katika kuongeza Shahada ya Uzamivu ambapo kwa sasa wanafunzi wanaendelea na masomo yao kikamilifu pamoja na kusaidia kufundisha watumishi katika maeneo tofauti kama watawala kupata nafasi ya kusoma nchi za nje.
“Vilevile katika kuongeza thamani mazao wametusaidia katika kufundisha walimu wetu na wafanyakazi wetu lakini vilevile kufundisha hata watawala upande wa fedha, mipango na rasilimali watu ambao baadhi walipata nafasi kwenda Denmark kujifunza ambayo imesaidia kuongeza tija na utendaji umehimarika” amesema Prof Chibunda.
Pia ameiomba Serikali ya Denmark na DANIDA kuangalia namna ya kuendelea kushirikiana na SUA katika kusaidia kuwafikia wakulima, kuimarisha mafunzo, pamoja na tafiti katika maeneo mbalimbali Tanzania kupitia SUA hasa katika muda wa miezi tisa iliyobaki ili kukamilika kabisa kwa mradi huo.
Nae mmoja wa wanufaika wa Mradi huo SUA ambaye ni Mhadhiri Msaidizi Bi. Judith Varelia amesema yeye amenufaika mara mbili kupitia mradi huo kwa kupata ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamivu na kufanya Miradi mbalimbali na hiyo imempa matumaini ya kumaliza shule kwa wakati na mwanga wa kujiona mtafiti mkubwa katika maeneo mengine.
“Naweza kumaliza shule yangu kwanza kwa wakati kwa sababu fedha ya kumalizia ipo lakini naona kuna uwezekano mkubwa zaidi wa mimi kuja kuandika zaidi kuhusiana na sekta zingine kutokana na ujuzi ambao nimeupata kipindi hiki nnachosoma Shahada ya Udaktari wa Falsafa yaani PHD hata hii PHD nnayosoma ni zao la mradi huu” amesema Bi. Judith Varelia.
0 Comments