Na Farida Mkongwe
Watumishi 28 kutoka Bohari Kuu ya
Dawa nchini (MSD) ambao wanakaribia kustaafu wametembelea Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kujionea, kupata elimu na kujifunza kwa
vitendo shughuli mbalimbali za Kilimo na Ufugaji zinazofanywa Chuoni hapo ikiwa
ni mojawapo ya maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Utumishi wa Umma ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo kwa watumishi wanaojianda kustaafu Bw. Livin Leon akizungumza na SUAMEDIA kuhusu ziara ya Watumishi wanaojiandaa kustaafu kutoka Bohari Kuu ya Dawa (Picha zote na Ayoub Mwigune)
Akizungumza na SUAMEDIA Februari 8,
2023, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya ambaye
ni Mratibu wa ziara hiyo Livin Leon amesema lengo lao kubwa ni kumuandaa Mtumishi
ambaye anajiandaa kustaafu aweze kuzijua
fursa mbalimbali zinazompa mwangaza mtumishi kuhusu maisha baada ya kustaafu.
“Tunamuandaa Mtumishi ajue kwamba
muda ukifika nitaagana na utumishi wa Umma, nitaenda kuanza maisha mengine nje
ya Utumishi wa Umma hivyo tumeshawaandaa kisaikolojia ili waweze kupokea hali
hiyo, na tutaendela kufanya hivi kwa sababu hili ni kundi la kwanza wiki ijayo
watakuja watumishi wengine”, amesema Mratibu huyo.
Amefafanua kuwa watumishi hao
wameshiriki kwenye mafunzo ya maisha baada ya kustaafu kwa siku 3 mkoani
Morogoro na hivyo wameona ni vema wakafika SUA ili wapate nafasi ya kujifunza
kwa vitendo na kwamba wamechagua SUA kwa sababu wameona ndio sehemu sahihi
yenye Wataalam waliobobea na wenye weledi katika masuala yahusuyo kilimo na
ufugaji.
Watumishi wanaojiandaa kustaafu kutoka Bohari Kuu ya Dawa wakiangalia Bwawa la Samaki lililopo SUA
“Tumechagua SUA kwa sababu
watumishi wanaweza kujifunza namna ya kuendesha Miradi mbalimbali kwa mafanikio
kutokana na Wataalam waliopo lakini pia ni sehemu ya kutengeneza network kati ya hawa watumishi na Wataalamu
wa SUA ili ikifika muda wa kuanza hili jambo basi waweze kuwatumia hawa
wataalam”, amesisitiza Mhadhiri huyo.
Kwa upande wao wastaafu hao
watarajiwa Steven Mafiri Yango kutoka Mara na Benjamini Hubila kutoka Dar es
Salaam wamewashukuru Wataalam wa SUA kwa kuwapatia mafunzo na maarifa ambayo
yatawasaidia wao na familia zao pamoja na jamii zinazowazunguka.
Katika ziara hiyo Watumishi hao
walitembelea Shamba la Mafunzo katika Kitengo cha Samaki, Kitengo cha Wanyama
na Kitengo cha Bustani na Mbogamboga kinachojihusisha na uzalishaji wa Mbogamboga
na matunda, Miche ya viungo mbalimbali pamoja na Maua.
Watumishi wanaojiandaa kustaafu kutoka Bohari Kuu ya Dawa wakiwa katika picha mbalimbali na wataalam kutoka SUA
0 Comments