Na: Farida Mkongwe
Watumishi kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini MSD ambao
wanajiandaa kustaafu utumishi wa Umma wamekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo SUA kwa kutoa Elimu ya Kilimo na Ufugaji ambayo imekuwa ikiwanufaisha
wakulima wengi nchini.
Shukrani hizo zimetolewa na baadhi ya watumishi hao wa MSD
wakati walipofanya ziara ya mafunzo chuoni hapo yenye lengo la kuwawezesha
kupata elimu na kuzitambua fursa zilipo SUA ambazo zinaweza kuwaongoza katika Miradi
mbalimbali watakayoianzisha katika kipindi hiki cha maandalizi ya kustaafu.
Wakizungumza na SUAMEDIA Februari 16, 2023 Bi. Mary Mshanga
kutoka Kilimanjaro na Manyema Nicholaus Mpangala kutoka Iringa wamesema ziara
hiyo imekuwa ni yenye mafanikio kwa sababu wamekutana na Wataalam wa SUA upande
wa Shamba la Mafunzo na kujifunza kuhusu ufugaji wa Samaki, Ng’ombe wa Maziwa, Mbuzi
na Kondoo lakini pia wamepata elimu kuhusu Kilimo cha Bustani ya Mboga mboga na
Matunda pamoja na Miche viungo na Maua.
“Tunawapongeza SUA kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuelimisha
jamii kuhusu masuala ya kilimo, mimi nimejifunza ufugaji wa samaki nimeweza
kujionea hatua kwa hatua namna vifaranga vya samaki vinavyozalishwa, pia
nimejifunza kuhusu ng’ombe wa maziwa na mambo mengine mengi, kwa kweli
tunamshukuru mwajiri wetu kwa kutupatia fursa hii ya mafunzo”, amesema Bi.
Mary.
Akitoa shukrani kwa SUA kwa niaba ya watumishi hao, Mhadhiri
Msaidizi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya ambaye ni Mratibu wa
ziara hiyo Bw. Livin Leon amesema wameamua kujifunza kutoka SUA kwa sababu SUA
ni Chuo cha Serikali chenye wataalam wa fani zote katika masuala ya kilimo na
ufugaji.
Awali akitoa mafunzo kwa watumishi hao Msimamizi wa Shamba la
Mafunzo Kitengo cha Bustani na Mbogamboga Roman Mfinanga aliwaeleza watumishi
hao kuwa ili waweze kulima kwa tija ni lazima wazingatie mambo matatu ambayo ni
kuwa na chanzo cha maji ya kutosha, kujua aina ya udongo na kuzingatia hali ya
hewa kwa sababu kuna mazao yanayostawi kwenye baridi na kwenye joto.
Hili ni kundi la pili la Watumishi hao wa MSD wenye umri wa kuanzia miaka 55 ambao wanajiandaa kustaafu kufika SUA kwa ajili ya kujifunza namna ya kuendesha Miradi mbalimbali iliyofanikiwa kupitia SUA, ambapo kundi la kwanza lilikuwa na watumishi 28 huku kundi hili la pili likiwa na watumishi 30.
0 Comments