SUAMEDIA

Wakulima wa Maharage washauriwa kutumia matandazo ya Viwandani ili kuongeza tija.

 

Na: Amina Hezron – Zanzibar.

Matokeo ya utafiti yaliyofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Chakula, Kilimo na Lishe (FoodLAND) yameonesha kuwa matumizi ya Matandazo ya viwandani katika kilimo cha Maharage yameonekana kufanya vizuri ukilinganisha na matandazo ya asili ambapo uzalishaji wake umeonekana kuwa mkubwa na yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uotaji wa magugu shabani.

 Dkt. Boniface Massawe amabye ni mtafiti kutoka SUA kwenye Mradi wa FoodLAND akiongea na Mwandishi wetu Visiwani Zanzibar kuhusu utafiti huo wa matumizi ya Matandazo.

Hayo yameelezwa na Mtafiti kutoka SUA Dkt. Boniface Massawe alipokuwa akizungumza na SUAMEDIA wakati wa Mkutano Mkuu wa tatu wa Mwaka wa Mradi wa Chakula Kilimo na Lishe (FoodLAND) uliofanyika Visiwani Zanzibar na kusema kuwa katika utafiti huo yalitumika matandazo ya asili, matandazo ya viwandani na sehemu nyingine hayakutumika kabisa.

“ Wakati tunafanya uangalizi baada ya uotaji tukagundua kwamba lile eneo ambalo lina matandazo ya viwandani halikuwa na nyasi nyingi magugu hayakuota kwa wingi lakini lile eneo ambalo halikuwa na matandazo kabisa lilikuwa na magugu kwa wingi sana huku pale tulipoweka matandazo ya nyasi na mikunde kunde napo magugu yaliota kidogo lakini siyo kwa kulinganisha na lile eneo ambalo halikuwa na matandazo kabisa”, alisema Dkt. Massawe.

Dkt Massawe ameeleza kuwa japokuwa uotaji wa mimea ya maharage katika sehemu isiyokuwa na matandazo kabisa ulikuwa mkubwa lakini hayakuweza kufikia uzalishaji ambao ulipatikana katika sehemu ambazo zilikuwa na matandazo.

“Hivyo tumejifunza kwamba uotaji unaweza ukawepo lakini uzalishaji usiwe mzuri  kama tulivyoona kuwa pamoja na huku kwenye matandazo haya ya viwandani uotaji ulikuwa hafifu lakini bado uzalishaji ulikuwa mkubwa ukilinganisha na uzalishaji katika haya matandazo mengine ambayo ni ya asili na lile eneo ambalo halikuwa na matandazo kabisa “, alisema Dkt Massawe.

Hivyo Dkt. Massawe amewashauri wakulima kujitahidi kutumia matandazo ili kuongeza uzalishaji kwakuwa hata katika jaribio hilo lilionesha kuwa uzalishaji wa maharage ulikuwa  mkubwa zaidi katika eneo ambalo lilikuwa na matandazo ya viwandani ikifuatiwa na eneo lenye matandazo ya mikunde kunde na nyasi .

Mkuu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Suzan Nchimbi Msolla akizungumza na Mwandishi wetu hii karibuni nje ya mkutano huo.

Naye Mkuu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Suzan Nchimbi Msolla ameeleza kuwa njia hiyo ya kutumia matandazo inasaidia kuhifadhi unyevu shambani lakini pia kwa kutumia aina hiyo ya matandazo aina ya kama plastiki kutoka viwandani itawasaidia wakulima kuondokana na matumizi ya matandazo ya plastiki ambayo hayaozi.

“Sisi tumejaribu na aina hiyo ya tandazo ambalo unaweza ukaliweka shambani na baada ya muda mara tu baada ya kuvuna mazao yako linaoza kabisa na kuchanganyika na udongo na linakuwa halina madhara kwa udongo”, alisema Prof. Msolla.

Post a Comment

0 Comments