SUAMEDIA

Mkoa wa Njombe waiomba SUA na TARI kusaidia kufufua kilimo cha ngano mkoani humo.

 Na: Amina Hezron - Njombe

Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omary amekiomba Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kuendelea kushirikiana na  Mkoa huo katika Mkatati wake wa kulifufua zao la Ngano na kulifanya kuwa zao la kimkakati ili liweze kuisaidia jamii  katika kuinua kipato chao  na Taifa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omary akiongea na Timu hiyo ya watafiti kutoka SUA na TARI ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Bi. Judica amezungumza hayo ofisini kwake alipotembelewa na timu ya Watafiti  na wataalamu wa maswala ya udongo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Taaisisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) waliokywa wanatembelea maeneo ambayo yanaanzishwa kama mfano Mkoani humo kwa Kilimo cha zao hilo.

“Halmashauri zetu zote nafikiri tayari wameshapewa maelekezo wanunue zile mashine za kupima udongo, lakini tunaamini kwa utafiti wenu pia mtatupatia nyinyi kama wataalamu wabobevu matokeo mmeona ardhi yetu  ipoje maana tumeambiwa ni muhimu sana pia kuangalia mbegu nzuri inayohitajika, upatikananji wa mbolea na namna ya kukifanya vizuri kilimo hicho”, alisema Bi. Judica.

Aidha Judica ameeleza kuwa wangependa kuona vijana wengi nao wanaingia katika kilimo hicho cha ngano na wamewashirikisha wakurugenzi ili kuona kama itawezekana katika asilimia kumi ya pesa za mikopo inayotolewa kuipa kipaumbele kuwawezesha katika uzalishaji waingie kwenye kilimo hicho na bila kusahau ufugaji na uvuvi .

“Zile asilimia kumi ziende kwenye vitu ambavyo ni vya muda mrefu na ikiwezekana tuwawezeshe vijana waweze kuingia kwenye kilimo, kwahiyo hili tunaona linaendana vizuri sana na anachokiongea Mhe.Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassani kwamba  sasa hivi tuwakusanye vijana ,tuwatafutie maeneo waende kwenye kilimo”,alisema Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Njombe.

Aidha amesema ikiwezekana SUA itengeneze program ambayo wakulima watakuwa wanapata mafunzo au wanakwenda SUA kufundishwa na kufanya mazoezi ya vitendo.

Nae Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Upande wa Taaluma,Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amemhakikishia Katibu tawala huyo wa Mkoa ushirikiano katika kutimiza nia hiyo kubwa.

Amesema SUA kupitia watafiti wake nguli kwenye eneo la Utafiti wa kilimo na sayansi zinazoendana na hizo watakuwa tayari kutoa ushauri wao wa kitaalamu katika nyanja zote za Kilimo,Mifugo,Mkusaidia kwa hali na mali utekelezaji wa mipango mbalimbali ya mkoa hiyo katika kilimo

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa Kituo cha (TARI) Mlingano Dkt. Catherine Senkoro ambae alizungumza kwaniaba ya wataalamu wa udongo ambao walifika Makete kwaajili ya vipimo vya udongo ameushukuru Mkoa wa Njombe kwakuhusisha taasisi za kiserikali za TARI na SUA katika kutekeleza malengo ya Taifa.

“Ni eneo ambalo linafaa kuna changamoto tu ambazo tunategemea hizi timu zote mbili tutaweza kutoa mapendekezo ya namna ya kuleta tija katika lile zao na kupunguza uingizaji wa  ngano katika nchini yetu lakini pia kukuza uchumi wa mkulima”, alisema Dkt. Senkoro.


Picha ya pamoja ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na Timu hiyo ya watafiti kutoka SUA, TARI,Chuo kikuu cha Dodoma  na Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark.
Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma,Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala (wa pili mbele) akifafanua jambo kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Jeremy Kusiluka.








Post a Comment

0 Comments