Na: Hadija Zahoro
Mkakati mpya 'Building a Better Tomorrow' (BBT) unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko utawawezesha vijana kujiajiri na kupambana wenyewe.
Mhadhiri na Mtaalamu wa Kilimo , Ufugaji na Uvuvi wa SUA, Dkt. Renalda Mnubi, wakizungumzia mjadala wa kuangazia kilimo cha Tanzania uliolenga kuwapatia fursa vijana kupitia mkakati huo. |
Hayo yameelezwa na Mhadhiri na Mtaalamu wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi wa SUA, Dkt. Renalda Mnubi, wakati akizungumza Mubashara na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) wakiwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakizungumzia mjadala wa kuangazia kilimo cha Tanzania uliolenga kuwapatia fursa vijana kupitia mkakati huo.
Dkt. Mnubi amesema kuwa kila mwaka kuna wanafunzi zaidi ya 200 wanahitimu katika kozi mbalimbali ikiwemo za kilimo kitu ambacho kinaupa ugumu serikali kuajiri wahitimu wote.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Kilimo Uchumi, Dkt. Zena Mpenda amesema kuna 60% hadi 70% ya vijana wanaohitmu wanaongezeka kila siku kwenye nguvu kazi inayohitajika, wameonekana kuishi chini ya mstari wa umasikini ambapo kunapelekea kutengeneza vibaka na wezi hivyo mkakati huo umekuja kuwa suluhu ya kuondoa umasikini kwa sababu utaajiri watu wengi nchini wakiwemo vijana.
Naye Mtaalamu wa Kilimo Biashara ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi SUA Dkt. Furgency Mishiri, ameeleza kuwa mkakati huo ni mzuri kwa serikali na vijana kwa sababu ya fursa zinazoenda kupatikana kutokana na utekelezaji wa mkakati huo.
‘‘Katika sekta ya kilimo mara nyingi tunaangalia mnyororo wa thamani ya mazao kutoka shambani mpaka mazao yanapomfikia mlaji hivyo, ukiangalia kuna sehemu nyingi katika mnyororo huo ambapo vijana wanaweza kuingia ikiwemo fursa nyingi za ajira kwa ajili ya kupata kipato’’, anasema Dkt. Mishiri.
“Ilizoeleka kuwa mkulima lazima avae nguo chakavu lakini sasa hivi nyakati zimebadilika ambapo wapo vijana ambao nawafahamu wanahamasika ambapo wamemaliza Shahada zao na wanafanya kilimo pamoja na biashara kama vile kuchoma mahindi jambo ambalo linampa faraja, anaeleza Dkt. Mishiri.
Naye, Mhitimu wa SUA na aliyekuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi 2021/2022, Mwita Mroni amesema kuwa hawawezi kusema kuwa wanategemea ajira kwa sababu kusomea kilimo ni ajira tosha hivyo wanatumia taaluma hiyo kuhakikisha kuwa wanajiajiri wenyewe kwa kushirikiana na vijana wenzao.
Ameeleza kuwa Serikali kupitia BBT ni mkakati mzuri ambao utekelezaji wake utakwenda kuleta matunda mazuri katika taifa la Tanzania hivyo, maono ya mkakati huo yakienda kutekelezwa ipasavyo yatazalisha kilimo endelevu na stahimilivu.
0 Comments