SUAMEDIA

'Lindeni Maadili na Utamaduni wa Kitanzania'" - Mhe. Nape


Na: Farida Mkongwe

Maafisa Habari na Mawasiliano kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Umma wametakiwa kuandaa Vipindi vya Elimu kwa Umma vitakavyolinda maadili na utamaduni wa kitanzania kama njia mojawapo wa kukuza na kuendeleza utamaduni nchini na kukabiliana na kasi ya kuenea kwa tamaduni za kigeni.


Wito huo umetolewa Februari 24, 2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Nape Nnauye wakati akifunga Mkutano wa 107 wa Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwaUmma mjini Morogoro.

Mh. Nape amesema mitandao ya kijamii kwa sasa ndio inayotumika zaidi katika upashanaji wa habari na kwamba ndani yake inakuja na tamaduni ambazo ni tofauti na maadili ya kitanzania hivyo kuna kazi kubwa ya kuhakikisha utamaduni wa Tanzania unalindwa ipasavyo.

“Nimeambiwa mmefundishwa mada mbalimbali, naamini mtayatumia mafunzo haya kama chachu ya mabadiliko katika majukumu yenu ambayo yanawekeza katika uzalishaji wa Vipindi vya Elimu kwa Umma, mkayatumie mafunzo haya kulinda utamaduni wa nchi yetu”, amesema Mh. Nape.

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba amesema TBC imekuwa ikiandaa mkutano huo kila mwaka kwa lengo la kuwajengea uwezo Maafisa Habari na Mawasiliano ili kuendana na kasi ya Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ambayo yanatokea duniani kote kwa sasa.

Miongoni mwa mada zilizofundishwa katika Mkutano huo ni Uandishi wa Ushawishi katika Mawasiliano ya Umma, Mawasiliano ya Kimkakati, Masoko Mtandaoni, uandaaji wa vipindi vya Luninga, ubunifu katika Maudhui ya mitandao ya kijamii pamoja na mada ya Uzalendo katika muktadha wa dunia ya sasa.

Mkutano huo uliobeba Kauli Mbiu isemayo “Vyombo vya Habari chachu ya Miradi ya Maendeleo” umeshirikisha jumla ya Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwa Umma 135 ambao wamepewa vyeti vya ushiriki.







   


Post a Comment

0 Comments