Na Ayoub Mwigune
Imeelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimejidhatiti kuwatengezea wanataaluma wapya mazingira mazuri na rafiki ya kazi ili kutimiza majukumu yao kikamilifu wawapo chuoni.
Hayo yameelezwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala wakati akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda , kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo wanataaluma wapya kwa ngazi ya wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataaluma ili waweze kuwa na mbinu na uwezo wa kutenda kazi kwa ufanisi.
Awali Prof. Mwatawala amesema kuwa lengo la
mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi katika usimamizi wa masomo pamoja na kuwasaidia
wanataaluma hao kuwa na uwezo wa juu wa kusimamia kazi za wanafunzi katika
majukumu yao ya kitaaluma.
Wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataaluma wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo
Aidha amesema Chuo hicho kitaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wanataaluma hao ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ya kazi kwa urahisi wawapo chuoni hapo.
Prof. Mwatawala amesema ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo kupitia Kitengo cha Udhibiti Ubora kitaendelea kuandaa warsha kama hizo zenye dhana mbalimbali ili kuhakikisha uwezo wa wanataaluma unaongezeka katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kitengo cha udhibiti Ubora Chuoni hapo Prof. Gration Rwegasira ameshukuru Mradi wa HEET kwa kuwezesha kwa asilimia kubwa mafunzo hayo ambapo zaidi ya wafanyakazi 80 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo .
Washiriki katika mafunzo hayo Bw. Mbonea Mwita na
Rejoice Otaru wamesema mafunzo hayo yatawasaidia namna ya kushi wakiwa kazini
kama wanataaluma, kutambua haki zao pamoja na namna ya kuweza kuwasiliana
vizuri na wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataaluma (mbele waliokaa ni viongozi mbali kutoka SUA)
Aidha wameishukuru menejimenti ya Chuo kwa
kuandaa mafunzo hayo ya siku tano pamoja
na mradi wa HEET kwa kuwezesha mafunzo hayo.
0 Comments