Na: Calvin Gwabara – Katavi.
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Nape Moses Nnauye amewahakikishia wanajumiya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda na wananchi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi kupata mawasilino ya uhakika wa simu pamoja na redio kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.
Mhe. Nnauye ameyasema hayo Januari 9, 2023 alipotembelea kampasi hiyo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi na viongozi wakuu wa mashirika yaliyo chini ya wizara yake kama vile TTCL, TCRA, UCSAF, TBC na mengine kwenye mikoa ya mpakani mwa Tanzania kuangalia usikivu na huduma za mawasiliano zilivyo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.
Amesema
Dunia ya leo mawasiliano ndio kila kitu na huko mbeleni swala la mawasiliano litakuwa
kitu kingine kikubwa na kwamba itafika mahali kutokuwa na mawasilino ni sawa na
kutokuishi ndo maana wameanza kuzungumza kuwa huduma za mawasiliano ni haki za
binadamu kwa kuwa vinakufanya uendelee kuishi.
“Kwenye
elimu ndio kabisa maana kwenye kazi za tafiti kama za kwenu hapa SUA usipounganishwa
na mawasiliano utashindwa kufanya kazi na kutimiza wajibu wako sawasawa, hapa
kwenu mnayo huduma kidogo ya TTCL na nimekuja na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL aseme
mwenyewe atafanya nini maana maagizo yalitoka kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo
Pinda lazima yatekelezeke, na Mbunge wa Jimbo hili ambaye ni Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria akinigomea mambo yangu hayaendi kwa hiyo kwa vyovyote lazima
tuondoke na majibu ya namna ya kumaliza tatizo hili na litaisha lini ili
nikampe majibu Mhe. Pinda” Ameseza Mhe. Nape.
Aliongeza “Siku moja nilikutana
na mzee wangu Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Pinda akaniambia kwenye kata ya Kibaoni sasa kuna Kampasi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo na imepewa jina lake lakini wanahangaika sana kupata mawasiliano maana mtandao
ni wa shida sana na mimi ndio Waziri wa Habari, nikamwambia Mzee nimekusikia
ngoja nione nitafanyaje” alieleze Mhe. Nape.
Akitoa majibu ya namna ya kumaliza tatizo hilo Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi. Peter Ulanga amesema kwa sasa wataboresha huduma ya mtadao wanaotoa kwenye kampasi hiyo lakini wataleta Mkongo wa Taifa kutoka kwenye kituo chao cha Kizi hadi kufika chuoni hapo na kukamilisha mpango huo kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.
“Sisi kama Shirika la Mawasiliano
nilishakuwa na kikao na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Raphael
Chibunda kule kampasi Kuu wameshatupatia mpaka eneo la kujenga Community WiFi
ambapo tunaweka WiFi mahali na wanafunzi wanaweza kuitumia, hivyo kwa umuhimu
wa Kampasi ya Mizengo Pinda na ombi lako Mhe. Waziri ukiruhusu tutafanya hivyo
pia na hapa kwenye kampasi hii lakini pia kama uongozi wa Chuo utatupatia eneo
hapa tutajenga mnara kwa ajili ya mawasiliano kwa maana ya matumizi ya simu na
line za TTCL 2G, 3G na 4G na tukaomba mnara huohuo TIGO nao wafanye co-
location” Alieleza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba amesema ni jukumu
la taasisi yake kupeleka huduma za mawasiliano vijijini maana makampuni ya simu
yanaona kuna baadhi ya maeneo ya vijijini hayapati faida kwa hiyo serikali
inaongeza ruzuku kidogo ili watanzania wa maeneo hayo wapate huduma za
mawasiliano.
Amesema kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwenye maeneo mengi na katika kata ya kibaoni anayo taarifa kuwa mtandao wa VODACOM unapatikana kwenye eneo hilo lakini kwa speed ya 2G ambayo ni kwa ajili ya kupiga simu tuu lakini haiwezi kutumia simu kubwa na ameongea nao wamemuahidi kabla ya mwezi wa pili watakuwa wamesha kukuza mawasilino na kwenda kwenye 4G ambayo itawawezesha kutumia simu janja zote vizuri na mtadao.
Awali akisoma taarifa fupi ya
Kampasi hiyo Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani amesema pamoja
na mafanikio makubwa yaliyopatikana toka kunzishwa kwa kampasi hiyo mwaka 2019
pamoja na matarajio makubwa waliyonayo katika kushiriki kwenye kuleta mageuzi
kwenye sekta ya Elimu na Kilimo nchini
lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa ya mawasiliano.
“Kutopatikana kwa mawasiliano kabisa ya Mtandao wa TIGO na TTCL na hivyo kusababisha kukosa njia mbadala ya mawasiliano, pili chuo kina mnara mdogo wa mawasiliano wa TTCL kwa ajili ya kunasa mawimbi ya internet lakini kasi yake ni ndogo na wakati mwingine mtandao haupatikani kabisa lakini pia mtandao sio wa uhakikwa kupitia mitandao ya simu na hivyo wanafunzi kushindwa kutumia maktaba za kimtandao na vyanzo vingine vya kujipatia machapisho na vitabu na walimu walioko kampasi kuu kushindwa kufundisha kwa masafa kupitia Zoom” Alieleza Prof. Katani.
Waziri wa Habari
Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Nape Moses Nnauye akiwa kwenye picha ya pamoja
na Wafanyakazi wa SUA Kampasi ya Mizengo Pinda. |
Wanajumuiya ya SUA Kampasi ya Mizengo Pinda, Wananchi wa Kibaoni,Viongozi mbalimbali wa CCM na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wakifuatilia mkutano huo. |
Wanajumuiya ya SUA Kampasi ya Mizengo Pinda, Wananchi wa Kibaoni,Viongozi mbalimbali wa CCM na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe wakifuatilia mkutano huo. |
0 Comments