Na Gerald Lwomile
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa rasmi zuio la mikutano ya
hadhara ya kisiasa nchini na kuwa sasa mikutano hiyo itafanyika kama Katiba ya
nchi inavyosema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza Ikulu Jijini Dar es Salaam (Picha TBC)
Rais ameondoa zuio hilo
leo Januari 03, 2023 Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na
viongozi wa vyama vya siasa na kusisitiza kuwa ni muhimu kuwepo kwa amani nchini.
Amesema ni wajibu wa
Serikali kulinda mikutano hiyo ya kisiasa lakini pia ni wajibu wa vyama vya
siasa kufuata taratibu zilizowekwa na kuwa ni muhimu kufanya siasa za kujenga
na si kubomoa.
“Kwa sheria zetu ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara……, kwa hiyo uwepo wangu mbele yenu hii leo nikuja kutoa ruhusa, kuja kutangaza kuwa lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa tumeliondoa” amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha Rais ameonya matumizi
ya lugha katika majukwaa ya kisiasa na kusema lugha za matuzi na kashfa si
sahihi kisheria na hata mila na desturi za mtanzania na atakayekwenda kinyume
na hayo basi sheria itachukua mkondo wake.
Akizungumzia suala la
Katiba, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa yeye na chama chake kimedhamiria kukwamua
mchakato wa marekebisho ya Katiba na kuwa bado kumeendelea kuwepo kwa
majadiliano ili kujua nini kifanyike kuhusu jambo hilo.
Amesema Katiba
itakayoundwa ni ya watanzania wote na si wanasiasa pekee na kuwa kutaundwa
kamati ambayo itahusisha makundi
mbalimbali, na kuwa sasa madai ya muda mrefu ya wanasiasa yanaanza kushughulikiwa
ili kuhakikisha kunakuwa na amani nchini.
0 Comments