SUAMEDIA

SUA kupitia mradi wa HEET yatoa mafunzo kwa Wanataaluma

 Na Jaqueline Japheth

Chuo kikuu cha Sokoine Cha Kilimo kupitia Kitengo cha Udhibiti Ubora pamoja na Mradi wa HEET wamewezesha mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo wanataaluma wapya kwa ngazi ya wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataaluma ili waweze kuwa na mbinu na uwezo wa kutenda kazi kwa ufanisi.


Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam Prof. Maulid Mwatawala akisisitiza jambo katika mafunzo ya kwa wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataaluma

Hayo yamebainishwa siku ya ufunguzi wa mafunzo hayo Januari 09, 2023 na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam Prof. Maulid Mwatawala wakati akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano yanayofanyika SUA Kampasi ya Edward Moringe, ukumbi wa Taasisi ya kujiendeleza Kielimu

Prof. Mwatawala amesema kuwa, Menejimenti ya Chuo inajidhatiti ili kuona kuwa Wanataaluma wanakuwa na mazingira mazuri ya kazi na kutimiza majukumu yao kwa urahisi pindi wawapo chuoni. Hivyo mafunzo hayo yatawasaidia katika kushughulikia mambo mbalimbali watakayo kutana nayo chuoni hapo.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Udhibiti Ubora Prof. Gration Rwegasira amesema kuwa, Kitengo kimeona umuhimu wa mafunzo haya kwa watumishi hao wapya ili kuwawezesha kufanya kazi zao katika ubora unaohitajika.  Kitengo hicho ambacho kipo chini ya ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo kina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba katika kila huduma inayotolewa Chuoni hapo inaendana na ubora ambao ulitarajiwa.



Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam Prof. Maulid Mwatawala (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataalum, wengine waliokaa ni viongozi mbalimbali wa SUA

“Tunahitaji SUA iendelee kuwa Chuo bora lakini kiwe Chuo kinachozingatia misingi ya kazi, kinachozingatia utu na vilevile kinachoendana na teknolojia ya sasa na ile ijayo. Tunataka wanachuo watakaohitimu SUA wawe na ubora ambao unahitajika huko Duniani” alisema Prof. Rwegasira.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa siku tano, yakihusisha masuala ya kiutawala, jinsi ya kuwahudumia wanafunzi na watumishi wenye uhitaji maalum, sera na sheria za SUA pamoja na mambo yanayohusu teknolojia ya habari.


 Wakufunzi wasaidizi na wasaidizi wa wanataalum wakiwa katika mafunzo

Post a Comment

0 Comments