Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo SUA, Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Taasisi ya Utafiti wa
magonjwa ya Binadamu NIMR, wamefanya utafiti na kuja na mapendekezo
yatakayowezesha kumaliza tatizo la minyoo tegu ya Nguruwe ambayo ina madhara
makubwa kwa afya ya Binadamu na Wanyama.
Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi na washiriki wa warsha hiyo ya kupokea na kujadili matokeo ya utafiti wa Mradi wa SYSTINET Afrika kuhusu Minyoo tegu ya Nguruwe inayofanyika Jijini Dodoma. |
Akifungua warsha hiyo ya kujadili mrejesho wa matokeo ya utafiti kuhusu namna ya kudhibiti minyoo tegu wa Nguruwe Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Ezron Nonga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia sekta ya mifugo Bwana Tixon Nzunda amesema Serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha matokeo ya utafiti huo yanatumika na kuleta tija kwa taifa.
“Tunapokuwa tunahitaji kutunga Sera
nzuri na kutekeleza mipango mbalimbali ya Wizara yetu tunathamini sana matokeo
ya tafiti maana yanatusaidia kupata uthibitisho na ushahidi ambazo zinawezesha
utengenezaji na utekelezaji wa miapango yetu kama wizara kwa maaslahi mapana ya
sekta ya mifigo maana yake huwezi kutengeneza Sera nzuri kama huna matokeo
sahihi ya utafiti” alisema Prof. Nonga.
Aidha amesema kwa mujibu wa
takwimu za mwaka 2022 Tanzania ina Nguruwe milioni 3.4 na inazalisha nyama tani
elfu 45 kwa mwaka, nyama ambayo inaonekana kuwa ndio nyama pendwa zaidi kuliko
nyama zingine kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Ezron Nonga akifungua Warsha hiyo. |
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Mifugo nchini amesema minyoo tegu ya Nguruwe inachangia ugonjwa wa kifafa kwa binadamu kwa zaidi ya asilimia 30 na hii ni kwa maeneo ambayo yanafuga Nguruwe kiasili nje ya mabanda kwa kuwaachia kujitafutia chakula wenyewe mitaani.
Akizungumzia matokeo hayo ya ujumla
wa tafiti hizo zilizofanyika kwa zaidi miaka 26 Mkurugenzi wa Mtandao wa
kisayansi wa CYSTINET Afrika Kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Helena Ngowi
amesema baada ya kazi kubwa ya utafiti kwenye maeneo mbalimbali nchini na
kupata matokeo wameona ni vyema sasa matokeo hayo na mapendekezo yao
wayawasilishe mbele ya wadau wote muhimu ikiwemo Wizara ili waone namna ya
kuyatumia katika kutunga sera zitakazosaidia kutokomeza Minyoo tegu hiyo.
“Baada ya kazi hii sasa tumekuja
na mapendekezo kadhaa ambayo tunaamini yakitekelezwa kwenye kipindi cha miaka
mitano tunaweza kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la Minyoo tegu ya
Nguruwe na kusaidia Jamii kufanya ufugaji bora na kula nyama salama ambayo
haiwezi kuleta athari kwa binadamu” alieleza Prof. Ngowi.
Mkurugenzi wa Mtandao wa kisayansi wa CYSTINET Afrika Kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Helena Ngowi akieleza malengo ya utafiti huo na hali ilivyo Tanzania. |
Ameyataja miongoni mwa
mapendekezo hayo ni kutengeneza Sera na miongozo au sharia ambayo itawafanya
wafugaji wote wa Nguruwe kufugia ndani ya mabanda badala a kuwaacha mtaani
wajitafutie chakula hali ambayo inasababisha mzunguko wa Minyoo tegu kuendelea.
Pia Mkurugenzi huyo wa Mtandao wa
kisayansi wa CYSTINET Africa amefafanua pendekezo linguine la utafiti huo kuwa
ni kuwepo kwa machinjio ya Nguruwe kwenye kila miji na vijiji ambavyo vinatumia,Vinafuga
au kufanya biashara ya nyama ya Nguruwe ili Nyama hiyo iwe inakaguliwa na
wataalamu waliopewa mamlaka ya kukagua usalama wa Nyama kuona kama ni salama na
haina minyoo hiyo ili kuzuia jamii kula nyma iliyoathirika.
Aidha Prof. Ngowi amesema kutoka
na kuwa na maeneo mengi ambayo watu wanakwenda kula nyama ya Nguruwe
wanapendekeza ziwe zinakaguliwa na kuwa safi ili kuondoa namna zozote za
uambukizaji wa wa mniyoo hiyo na kuhakikisha inapikwa vizuri katika viwango
vinavyotakiwa ili kuweka walaji kwenye mazingira salama wanapokula.
Amesema kwakuwa mayai ya Minyoo
ya Tegu wa Nguruwe yameonekana kwenye ardhi kwenye maeneo ya wafugaji wa
Nguruwe na yanaweza kuishi kwa muda mrefu kwenye ardhi na yakipata mazingira ya
kuanguliwa yanaanguliwa wamependekeza kuwe na maeneo ya maji safi kwaajili ya
kunawa mikono mashuleni na kwenye masoko ili kuepuka kula mayai hayo ya tegu
kutokana na vumbi au matunda nambogamboga sokoni.
Awali akizungumza kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii
na insia Prof. Samweli Kabote aliyemuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kwa upande wa SUA mradi huo
umejikita katika kufanya uchunguzi wa kina wa hali ya maambukizi pamoja na
kufungamanisha na utoaji wa elimu ya fya kwa gharama nafuu na kujenga uwezo wa
kitaasisi na kimfumo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kupitia mkakati wa
afya moja.
Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na insia Prof. Samweli Kabote aliyemuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo Prof. Raphael Chibunda akitoa salamu za SUA. |
“Nchini Tanzania, utafiti huu
umeoensha viwango tofauti vya maambukizi ya minyoo tegu kwa Binadamu na kwa
Nguruwe lakini pia tumeona jinsi ambavyo binadamu yupo katika hatari ya kubwa
ya maambukizi ikiwa hatozingatia usafi na matumizi sahihi ya vyoo au kula nyama
ya nguruwe yenye maambukizi” alieleza Prof. Kabote.
Aliongeza “Madhara ya minyoo tegu
ni makubwa ikiwemo Kifafa,Kupooza na
upofu hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari na kufanyia kazi mapendekezo
yaliyowasilishwa kwenye utafiti huu ili kuepukana na magonjwa hayo”.
Prof. Kabote amesema
kunamahusiano makubwa ya magonjwa hayo yanayotokana na minyoo tegu ya Nguruwe
na Maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya binadamu kwakuwa wanatashindwa kushiriki
kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo na uchumi na kuanzia ngazi yake binafsi
hadi Taifa.
Utafiti huo umefanyika kwenye
wilaya za mikoa mbalimbali inayosifika kwa ufugaji wa nguruwe ikiwemo Mbulu, Babati,
Songwe, Kongwa, Mpwapwa, Mpanda unatekelezwa kupitia mradi wa CYSTINET Afrika
kwa ufadhili wa Wizara ya elimu na utafiti ya shirikisho la Ujerumani (BMBF).
PICHA ZA WASHIRIKI WA WARSHA WAKIFUATILIA UWASILISHWAJI WA MATOKEO.
0 Comments