SUAMEDIA

Serikali yaahidi kuyafanyia kazi matokeo ya utafiti wa Minyoo tegu ya Nguruwe kulinda afya ya Jamii na mifugo.

 Na: Gladness Mphuru - Dodoma.

Pamoja na madhara makubwa yatokanayo na Mnyoo tegu wa nguruwe kwenye mwili na afya ya binadamu lakini bado magonjwa yatokanayo na Mnyoo huo yapo kwenye kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele na mashirika ya afya na taasisi zake.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga wakati akifungua warsha hiyo jijini Dodoma.

Hayo yamebainika Januari 25, 2023 Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo kwenye  Warsha ya kujadili mrejesho wa matokeo ya Utafiti kuhusu namna ya kudhibiti Mnyoo Tegu wa Nguruwe Tanzania.

“Na sisi Wizara ya mifugo katika nguruwe tuna ugonjwa mmoja tuu wa Homa ya nguruwe afrika hata huu wa tegu nao hatujaupa kipaumbele, kwahiyo ni wakati muafaka sasa kutokana na tafiti hizi ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi tuone kuwa ni kweli haujapewa kipaumbele lakini watu wetu wanaangamia” alieleza Prof. Nonga.

Prof. Hezron Nonga amesema warsha hiyo itasaidia Serikali,Wizara na Wadau wote  kupanga mikakati ya pamoja na endelevu ya kuzuia na kutokomeza kabisa mnyoo tegu wa nguruwe nchini kwa kuelimisha jamii kuepukana na vyanzo vinavyosababisha ugonjwa huo.

Aidha ameongeza kuwa wafugaji wa nguruwe wanaowacha kujitafutia chakula mitaani bila kufungiwa kwenye maeneo yanayofuga ambayo jamii haitumii vyoo kunapelekea Nguruwe kula kinyesi cha binadamu na mwenye maambukizi ya tegu ni kusabisha mzunguko wa maisha ya tegu kuendeela kwenye jamii.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi kutoka SUA, amesema madhara yatokanayo na Mnyoo Tegu kwa Binadamu kiafya ni Pamoja na Kifafa, Kupooza na Upofu wa Macho lakini pia kijamii wengine kukosa wake na waume wa kuwaoa pale wanapogundua familia ina historia ya watu wenye ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi kutoka SUA akiwasilisha mada kuhusu magonjwa yanayosababishwa na Mnyoo tegu na madhara yake kwa jamii nchini Tanzania.

Amesema katika utafiti huo wameangalia kiwango cha maambukizi na vichocheo vya maambukizi hayo ya mnyoo tegu kwa nguruwe na binadamu ambapo wamefanya kwa kushirikiana na Taasisi zingine katika dhana ya afya moja ili kuweza kupata mbinu za pamoja za kutokomeza minyoo hiyo.

Aidha, amesema ili kutatua athari zinazotokana na Mnyoo Tegu ameshauri elimu zaidi itolewe kwa jamii kujua mnyama aliyeathirika na njia za kudhibiti kuenea kwa minyoo hiyo na kuishauri serikali kuona uwezekano pia wa kuajiri wataalamu wengi wa mifugo ikiwezekana kila kata, mitaa na vijiji.

Kwa upande wake Mhadhiri mwandamizi kutoka SUA Dkt. Justin Maganila ambaye alifanya utafiti kuhusu afya ya chakula, uwepo wa vimelea kwenye ardhi kwenye maeneo yanayofuga nguruwe amesema wamefanikiwa kuelimisha jamii kwa baadhi ya maeneo nchini kuhusu Mnyoo Tegu ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma.

“Tunaishauri Serikali iweke Sera ambayo itaelekeza njia bora za ufugaji wa Nguruwe, matumizi ya vyoo na usafi wa nyama zile njia zote ambazo tukizitumia tutadhibiti ugonjwa huu, hata Shirika la Afya Duniani WHO) linasisitiza kuwa Mnyoo Tegu wa Nguruwe linadhibitika kwa kufuata kanuni hizo ambapo tutainua kipato cha mfugaji na hata taifa, pia afya za watu zitaimarika” alieleza Dkt.Maganila.    

Mradi wa Cystinet Africa ni mradi ambao umefadhiliwa na Wizara ya Elimu na Utafiti ya Serikali ya Ujerumani (BMBF) ambao umeratibiwa na SUA, Mtandao huu unajumuisha Taasisi 5 katika Nchi Nne za washiriki ambazo ni SUA, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania, Chuo Kikuu cha Zambia Pamoja na Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane - Msumbiji.

Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na insia Prof. Samweli Kabote aliyemuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo Prof. Raphael Chibunda akitoa salamu za SUA kwenye Warsha hiyo.







Post a Comment

0 Comments