Na: Amina Hezron na Calvin Gwabara – Zanzibar.
Imeelezwa kuwa matokeo yote
mazuri ya Mradi wa Chakula Kilimo na Lishe (FOODLAND) yaliyopatikana kwenye nchi
zinazotekeleza mradi huo yatakwenda kuisaidia jamii katika kuhusanisha Kilimo,
Matumzi ya mazao ya chakula na lishe na hivyo kupunguza changamoto za chakula na
lishe Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Makamu Mkuu wa Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu
Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua Mkutano Mkuu wa wa tatu wa Mwaka wa
Mradi huo uliofanyika visiwani Zanzibar wa kufanya tathimini ya kazi zilizofanyika
ndani ya mradi ili kuendelea kuboresha ufanyaji kazi wa mradi huo.
“Mradi huu unaunganisha kwanza uzalishaji wa chakula
lakini pia na matumizi ya chakula kwa sababu kumekuwa na miradi mingi ambayo
imekuwa ikiangalia uzalishaji tu pekee
na miradi mengine mingi ikiangalia matumizi ya chakula pekee kwa hiyo kunakuwa
hakuna muunganiko au uhusiano kati ya uzalishaji na matumizi ya chakula. Inawezekana chakula kinazalishwa sana
kuliko kinavyoliwa au kinacholiwa zaidi si kinachozalishwa kwa kiwango kile
ambacho kinahitajika”, alisema Prof Mwatawala.
Prof. Mwatawala amesema
amefurahishwa sana na Mchanganyiko wa wadau wanaotekeleza mradi huo kwa kuwa
unawahusisha Watafiti, Wajasiriamali na Wabunifu maana mwisho wa utafiti
matokeo hayo yatawahusu watu hao katika makundi yao na watatakiwa kufanya kazi
zao kwa kuzingatia matokeo yatakayopatikana kwakuwa ndio njia ya kufikia
mapinduzi ya nne ya viwanda.
Akizungumzia malengo ya Mradi wa
FoodLAND, Mkuu wa Mradi huo kwa upande
wa Tanzania Prof. Susan Nchimbi Msolla Kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
amesema unalenga hasa uboreshaji wa kilimo ili watu waweze kulima kilimo chenye
tija na kinachohifadhi mazingira na kuzingatia lishe.
“ Tunalenga kuoanisha kati ya
kilimo na lishe mara nyingi tumekuwa tukiona kwamba tunazalisha chakula kingi
sana lakini wakati mwingine sehemu hizo hizo zinazozalisha chakula kingi lishe
yao ni duni kwa hiyo sisi kwenye mradi huu tunataka tuweze kuoanisha uzalishaji
wa chakula ili nchi yetu iwe na watu
wenye lishe bora”, alisema Prof Msolla.
Aidha Prof. Msolla amesema kuwa
mradi huo unataka kuwa na Bioanuai ya vyakula na mazao yanayolimwa kwa kuwa
imekuwa ikionekana katika sehemu zingine kutokana na tabia za ulaji watu
wanakula vyakula vya aina chache ingawa
kuna uwepo wa vyakula vingi vinavyozalishwa huku vingine vikiuzwa na wenyewe
wanaozalisha hawavili.
“Tunataka tuweze kuongeza uwelewa
zaidi kwa wakulima na walaji na ndio maana katika mradi huu katika hatua zetu
za mwanzo tuliweza kufanya madodoso na wakulima na walaji wa vyakula mijini na
vijijini ili tuweze kujua tabia za ulaji zikoje na kwanini watu wanachagua
vyakula wanavyokula”, alisema Prof. Msolla.
Mtafiti huyo mkuu wa Mradi
ameeleza kuwa matokeo ya Utafiti huo yatasaidia katika kuboresha na kushauri watu
namna ya kulima, aina ya mazao ya kulima,kilimo cha aina gani kitumike na aina
gani ya vyakula watu wale ili kuboresha afya zao .
Akieleza kwa ujumla malengo ya
mradi ,utekelezaji wake mpaka sasa na Matarajio ya mbele Mratibu wa Mradi wa
FoodLAND kwa nchi zote washiriki Prof.
Marco Setti kutoka Chuo Kikuu cha Bologna cha nchini Italy amesema mkutano huo
ni fursa kubwa kwa washiriki wote kukutana pamoja na kubadilishana maarifa na
mbinu za utekelezaji ili kufikia malengo tarajiwa.
Amesema kumekuwa na maendeleo
makubwa na mazuri ya utafiti kwenye nchi zote wananchama kasoro Ethiopoa ambako
kuna kuchelewa kwa utekelezaji wa kazi mbalimbali kutokana na changamoto
mbalimbali za nchi hiyo lakini wana Imani kuwa nao watakamilisha na kupata
matokeo.
“Tayari tumeshazalisha takribani matokeo
30 na kuyawasilisha kwa wafadhili wetu ambao umoja wa Ulaya(European Union) ambayo yanapatikana
kwenye tovuti ya mradi na kwenye tovuti ya
Umoja wa Ulaya na kila mmoja anaweza kuyaangalia kujua kilichopatikana yapo
mengine 7 yaliyozalishwa mwezi mmoja uliopita na mengine matano yanayohusu
miongozo na zana za kufundishia yanaendelea kukamilishwa” alisema Prof. Seti.
Mradi wa FoodLAND ulianza kutekelezwa
mwezi wa tisa mwaka 2020, ukishirikisha wadau 26 kutoka nchi 13 ambapo za Afrika
inawakilishwa na Tanzania,Kenya,Uganda,Ethiopia, Tunisia, Morocco ambapo kwa
mara ya kwanza wanakutana Tanzania kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa mradi huo
baada ya miaka miwili yote kufanyika kwa njia ya mtandao kutokana na changamoto
za ugonjwa wa UVIKO 19.
0 Comments