Na; Gladness Mphuru
Chuo cha Taifa cha Ulinzi kimeahidi
kuwa Balozi wa mikakati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kutokana na
Chuo hicho kuwa na mikakati bora ya Kilimo cha Kibiashara ambayo itanufaisha
mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda (kulia) akimpa zawadi Mkufunzi Mwandamizi wa Jeshi la Nchi kavu, Brigedia Jenerali Stephen Mnkande wakati wa ziara ya maafisa wa Jeshi chuoni hapo (Picha zote na Gerald Lwomile)
Hayo yamebainishwa Januari 19, 2023 na Mkufunzi Mwandamizi
wa Jeshi la Nchi kavu, Brigedia Jenerali Stephen Mnkande, akiwa na ujumbe wake
wa Maafisa mbalimbali kutoka Jeshini na wengine kutoka nje ya nchi ikiwa ni siku ya kwanza kwa ziara ya siku
mbili, ambapo amepokelewa na mwenyeji wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof.
Raphael Chibunda.
Katika ziara hiyo wameweza kutembelea maeneo mbalimbali ya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo ni Kitengo cha Ukuzaji Viumbe Maji, Hospitali ya Rufaa ya Wanyama na Mradi wa Utafiti kwa kutumia Panya (Apopo)
Awali akijibu hoja mbalimbali baada ya kutoa
taarifa ya Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof.
Raphael Chibunda amesema Chuo hicho kimekuwa kikihakikisha kinatoa wahitimu
ambao wanaweza kwenda kuajiriwa lakini hata kama hawapati ajira basi wana uwezo
wa kujiajiri
Maafisa mbalimbali kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakiangalia naamna mnyama anavyofanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Wanyama iliyopo SUA
Amesema SUA imeboresha mafunzo yake ikiwa ni pamoja na kuanzisha mashamba darasa ambayo wanafunzi wanajifunza moja kwa moja
shambani kitu kinachoweza kuwasaidia kuanzisha mashamba na kufanya kilimo
chenye tija
Aidha Prof. Chibunda amesema SUA imekuwa
ikiwahamasisha vijana kuanzisha vikundi ambavyo kwa kushirikiana wanaweza
kupata mitaji na kufungua mashamba makubwa na kuwa na kilimo chenye tija
Ziara hiyo maofisa kutoka Chuo cha Taifa cha
Ulinzi na maafisa wengine kutoka nje ya Tanzania itaendelea tena Januari 20,
2023 katika Kampasi ya Solomon Mahlangu iliyo katika Manispaa ya Morogoro
Maafisa mbalimbali kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi wakitembelea maeneo mbalimbali SUA
0 Comments