SUAMEDIA

Wananchi watakiwa kuwahi hospitalini wanapong’atwa na mbwa

 Na Adam Maruma - Dodoma

Wanafunzi wa Shule za msingi Amani na Shule ya Sekondari Umonga zilizopo jijini Dodoma wamenufaika na elimu  ya kujikinga na Kichaa cha Mbwa iliyotolewa na Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA)  ambapo wanachama wa Chama hao kutoka ndani na nje ya nchi wanakutana jijini  humo kwenye   Kongamano la Kisayansi la mwaka lililoanza tarehe 5 Disemba 2022 na kufanyika kwa muda wa wiki nzima,  kwenye ukumbi wa Hazina jijini humo.


Dk. Harrison Gabriel akitoa mafunzo ya namna ya kujikinga na kupata huduma mtu anapong'atwa na Mbwa mwenye Kichaa

Timu ya Madaktari ilianza kwa kuitembela shule ya Msingi Amani,iliyopo jijini humo,  ambapo wanafunzi walifundishwa namna ugonjwa huo unavyohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa mbwa wanaozurura mitaani  na hivyo  uwezekano wa kushambuliwa na mbwa mwenye kichaa sababu mbwa mwenye ugonjwa huo anakua na ukali usio wa kawaida

Dk. Harrison Gabriel ni  mtafiti wa Mifugo Kanda ya Kati na ni mmoja  wa madakatari waliofundisha wanafunzi hao namna ya kumpa huduma ya kwanza mtu aliyeng’atwa na mbwa  kwa kuosha kidonda hicho na maji tiririka na kukiacha bila kukifunga na kitambaa , huku akisistiza kumuwahisha mgonjwa hospitali ili kuokoa maisha ya mgonjwa na ikiwa mgojnwa  atacheleweshwa kupelekwa hospitalini na kama mbwa aliyemng’ata mtu huyo atakua na kichaa kuna  uwezekano wa mgonjwa kupoteza maisha.

Daktari huyo mtafiti, pia amesema kuwa si kila mbwa anayeng’ata watu barabarani ana ugonjwa huo mara nyingine wanyama hao rafiki wa binadamu wanakua wamejeruhiwa kwa vipigo kutoka kwa baadhi ya watu  na kuwataka wanafunzi hao kuacha mara moja kuwachokaza mbwa anaowakutana barabarani au wakiwa wamefungwa majumbani mwao, na hivyo kuwaeleza  kuwataka  wenye wananchi wenye kufuga  mbwa kutowacha wanyama hao kuzurura mitaani.

Aidha mtafiti huyo  ameongeza kuwa  kama wafugaji wa mbwa watachanja mbwa wao kila mwaka na kuwatunza majumbani kwa kuwapa mbwa chakula pamoja kuwaweka katika mazingira mazuri ya kulala mbwa wanakuwa msaada mkubwa kwa ulinzi wa majumbani, kwa kua mbwa ni kati ya wanyama wanofundishika vizuri na kuwa uwezo wa kubaini endapo kuna ugeni mpya nyumbani hapo.

Mwl. Phidea Mapunda ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Umonga jijini Dodoma, na amesema amefurahia elimu iliyotolewa na Madakatari hao na  pia akatoa, ushuhuda wa namna shule moja ya jirani ilivyompoteza mwanafunzi wao, aliyeng’atwa na mbwa akiwa shuleni  na baadae mwanafunzi huyo kupoteza maisha kwa sababu walimu wa shule hiyo  kutokua na elimu ya kichaa  cha mbwa na kumchelewesha kumpeleka kituo cha Afya.

            Mwl. Phidea akipokea bango lenye elimu ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa

‘’Tunashukuru kwa Elimu hii Muhimu kwa Jamii,kuna tukio moja lilitokea shule moja ya jirani ya watoto wadogo, ghafla mbwa alitokea shuleni hapo na mwanafunzi aling’atwa na mbwa huyo, na kwakua jeraha lilikua dogo Walimu walimpatia mwanafunzi huyo Panadol na wakamruhusu aendelee na masomo hadi jioni,lakini jioni hali ya mtoto ikabadilika tena na wakampeleka Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya wiki mbili yule mwanafunzi alipoteza maisha’’ amesema Mwl. Phidea.

Afisa mifugo jiji la Dodoma Gratian Mwesiga  mwenyeji wa Madaktari hao, amesema njia kuu ya kudhitibi kichaa cha mbwa ni kichanja mbwa wote, lakini wao kama wataalum inawawia vigumu kujua hali ya mbwa wanaozurura mtaani kama wamechanjwa na hivyo kulazimika  kuua mbwa  wanaozurura ili kunusuru maisha ya wananchi.

Naye Dk. Kijida Gidioni Polisi, anayehudumia mikoa ya kanda ya Magharibi, katika  mafunzo hayo alifundisha wanafunzi hao namna ya kumtambua mbwa mwenye kichaa cha Mbwa na kuzitaja dalili kama, Mbwa kutoa  Mate mengi kinywani, kuogopa mwanga, pamoja  na kuogopa maji, mbwa kubadili kabadili tabia kama alikua mkali anakua mpole, na kwa upande wa binadamu aliyembukizwa  ugonjwa wa kichaa cha mbwa huwa na dalili za maumivu ya mwili, kuwashwa sehemu yenye jeraha, kuweweseka na kujificha na dalili zingine ni kuogopa kuoga na kupata nguvu za ajabu na mwili kupooza.

Kwa upande wake mwanafunzi wa Kidato cha Tatu shule ya Sekondari Umonga, Patrick Apolinary Mwacha amesema atafikisha elimu aliyoipata kwenye familia yake na jamii kwa ujumla kwa kuwa wananchi wengi wa  wanaoishi nje ya jiji la Dodoma ni wafugaji wa mifugo mbalimbali wakiwemo mbwa na kumekua na ufahamu mdogo wa namna ya kuepuka kichaa cha mbwa miongoni mwao mwa jamii hizo za kifugaji.


Wanafunzi mbalimbali wa shule ya Msingi Amani wakimsikiliza mwenzao aliyekuwa akijibu swali wakati wa mafunzo


Post a Comment

0 Comments