SUAMEDIA

Maafisa Mifugo nchini watakiwa kuhamasisha chanjo kwa mifugo.

 

Adam Maruma - Dodoma

Maafisa mifugo nchini wametakiwa kuwahamasisha wafugaji, kuchanja mifugo ili kuilinda  dhidi ya magonjwa mbalimbali ambayo yanatajwa kuwa ni moja ya kikwazo kikubwa kinachorudisha nyuma maendeleo ya mifugo nchini.



Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari ya Mifugo nchini Prof. Esron Karimuribo (kushoto) akipokea chanjo kutokwa kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania  Prof. Hezron Nonga

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga wakati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara Hiyo, wakati akipokea chanjo za kuzuia magonjwa mbalimbali ya Mifugo  nchini ili kuunga mkono jitihada za Chama cha Madaktari wa Mifugo nchini, watakaotoa huduma za elimu, chanjo na upasuaji  wa mifugo kwenye  Kata za Nala na Mbalawala zizizo nje kidogo ya Jiji la Dodoma .

Prof. Nonga amesema idadi ya mifugo nchini iliyochanjwa  bado ni ndogo kwani katika Halmashauri  184 nchini ,kuna baadhi ya Halmashauri hazichanji kabisa mifugo yao, lakini Madaktari wa mifugo wapo katika kata hizo, chanjo zipo na wafugaji wapo tayari kuzilipia huku akitaja sababu kuwa ni kutowajibika ipasavyo kwa baadhi wa Madaktari ya mifugo na maafisa ugani mifugo katika Halmashauri hizo.

Mkurugenzi huyo wa Huduma za Mifugo nchini, ameongeza kuwa ni muda wa Madaktari wa Mifugo nchini kufanya kazi kwa kujituma, kwani katika kata 3,956 nchini na vijiji zaidi 12,193 nchi nzima, nusu ya kata hizo zina maafisa mifugo ambao kwa wastani afisa mmoja anaweza kuhudumia vijiji angalau 2 hadi 3 katika kata moja, na kuweza kutoa elimu ya namna ya kudhibiti magonjwa ya Mifugo bila tatizo kwa kuwa wizara imewapatia  pikipiki zaidi ya 300, huku pikipiki 1,200 zikitarajiwa kutolewa mwaka huu  kwa maafisa ugani wa mifugo, na madaktari hao ili waweze kufanya kazi yao kwa urahisi.



Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akizungumza na wadau mbalimbali wa mifugo wakati akipokea chanjo hizo

‘’Wizara imeanzisha utaratibu wa kupima ufanyaji kazi wa maafisa ugani mifugo na madaktari wa mifugo, kuona kama uwepo wao kazini una tija kwa Serikali au wapo pale kwa ajili ya kupumzika huku Serikali ikendelea kulipa mshahara kwani Serikali haipo tayari kuendelea kulipa Misahara kwa wafanyakazi waliokuja  kupumzika makazini ’’, Amesema Prof, Nonga.

‘’Nishukuru kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazozalisha chanjo yake yenyewe, sasa hivi kuna viwanda vitatu vya kuzalisha chanjo ya mifugo, kuna kiwanda cha Serikali kinaitwa Tanzania Vaccine Insitute, chini ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania, na  kinazalisha Zaidi ya chanjo saba dhidi ya magonjwa kipaumbele”

Amezitaja chanjo hizo kuwa ni zaidi ya dozi milioni 65 kwa mwaka na hizi zinatumika mara moja na kuisha , Kiwanda binafsi cha NOVABI kinazalisha chanjo inaitwa Tatu Moja ambayo ni chanjo kuku na  imeunganisha magonjwa matatu ya kuku ndani yake ambayo ni Kideri, Ndui ya Kuku, pamoja na Mafua ya Kuku.

Chanjo nyingine zinazozalishwa ni dozi milioni 50 kwa mwaka  na kiwanda cha Wazalendo, lakini zaidi ya yote kuna kiwanda kikubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara  ambacho kinaitwa Hester Biosciences Africa Limited kiko Tanzania na kinatambuliwa na Dunia nzima na kinazalisha chanjo aina 37 dhidi ya magonjwa mbali mbali ya mifugo.

Kwa upande Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari ya Mifugo nchini Prof. Esron Karimuribo amewashukuru wawakilisha wa kampuni zilitoa chanjo mbali mbali za mifugo na namna  itakavyotumika katika kuhudumia wafugaji wa kata za Nala na Mbawala zilizo nje  kidogo ya jiji la Dodoma na kusema zaidi ya dozi 4,000  zitatumika kuchanja mifugo katika kata hizo.


Prof. Esron Karimuribo akizungumza katika hafla hiyo

Chanjo zilizotolewa katika makabidhiano hayo  ni za kuzuia magonjwa ya Sotoka, yambuzi na Kondoo, Chanjo ya kuzuia mapele ngozi ya na chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa  kwa ajili ya jiji la  Dodoma.



Post a Comment

0 Comments