SUAMEDIA

Wakazi, Wafanyabiashara wazungukao Kampasi ya Mizengo Pinda (SUA) Katavi tayari kuupokea Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET)

Na: Tatyana Celestine, Katavi


Wakazi na Wafanyabiashara wazungukao Kampasi ya Mizengo Pinda (SUA)  Katavi wamefurahia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) ambao umeanza kutekelezwa  kwa kufanya tathmini na kukusanya maoni kwa wadau wake ili kukamilisha malengo ya Benki ya Dunia katika hatua za ushirikishwaji na kuepusha malalamiko.


Mtaalam wa masuala ya Kijamii  Prof. David Mhando (kushoto) pamoja na Mtaalm wa Mazingira Dr. Amina Hamad wakizungumza na wanakijiji cha Kibaoni mkoni Katavi wakati wa kutathmini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya kiuchumi




Bi. Magreth Anselma ambaye anajishughulisha na Biashara ya kusuka nywele nje ya Kampasi hiyo ya Mizengo Pinda amesema kuwa wanayo furaha baada ya Wataalamu wa Mazingira na masuala ya Kijamii kuwafikia na kuondoa sintofahamu ambayo walikuwa nayo kwamba nyumba zao zitabomolewa lakini kwa sasa wametambua Mradi huo si wa kuja kuwarudisha nyuma kimaendeleo badala yake umekuja na fursa nyingi kwao kuweza kuinuka kiuchumi. 


Bi. Anselma ameongeza kuwa picha anayoiona kwa sasa ni kuwa wakazi hao na wafanyabiashara ni kuanza kujiandaa kuongeza mitaji ili majengo yatakapoanza kujengwa mafundi watakuwa ni wateja wao lakini pia Wanafunzi wakiongezeka watawawezesha kuongeza kipato, pamoja na kupata ajira kwa kusaidia ujenzi kitu kitakachowafanya nao kuweza kusomesha watoto wao.


Aidha Bi. Betrida Mwasapi ameongeza kuwa ni Mradi mzuri kwa maana hata watoto wao watasoma katika Chuo hicho na kusaidia kupunguza gharama tofauti na kupeleka watoto kusoma mbali na nyumbani hivyo watoto wao watakuwa salama kwani watakuwa wanawaona bila kutumia nauli kwenda mbali.


Nao Wamiliki wa Bwalo la Chakula katika eneo hilo wamefurahia Chuo cha SUA kufikiria kuongeza Bwalo kubwa Kwa ajili ya Wanafunzi kwani wao wameichukulia kama ushawishi  kwao kuboresha zaidi maeneo yao ya kibiashara ili kukabiliana na ushindani wa kibiashara utakaojitokeza mara baada ya Mradi huo kukamilika.


Akizungumzia namna ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara utakaotokana na utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi Prof. Ruwa-Aichi Temu amesema kuwa wafanyabiashara wajiandae vema na wanayo nafasi ya kubadili aina ya biashara kutokana na ongezeko la watu kwani kuna maeneo makubwa na hivyo ni rahisi kwao kuchangamkia fursa baada kufika kwa  Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi.


Kutokana na maboresho hayo yatakayoweza kubadilisha taswira nzima ya eneo hilo, Meneja wa Mgahawa na vyumba vya kupanga Bi. Pricila Venance amekishukuru Chuo kuonesha kuwajali wakazi na wafanyabiashara waliopo jirani na Kampasi ya Mizengo Pinda hasa kwa kutoa namna Bora ya kuwasilisha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kutekelezwa Mradi.


Aidha ameainisha changamoto hizo ikiwa pamoja na Unyanyasaji wa kijinsia, ulinzi wa watoto wao, wizi, usambazwaji wa magonjwa kiholela pamoja na kuwepo kwa tabia zisizofaa katika eneo hilo na kusema njia hizo zitawasaidia kuona wako salama na kuwa nao ni sehemu ya Mradi huo.


Kwa upande wa Mtaalam wa masuala ya Kijamii Prof. David Mhando amewatoa hofu wakazi na wafanyabiashara hao na kusema  wanatakiwa kushirikiana na Mradi katika kila hatua, kuwa walinzi kabla na baada kwani kufanikiwa kwa Mradi kutawaletea Mabadiliko na maendeleo na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza zaidi kitu ambacho ni mategemeo ya Benki ya Dunia na Chuo kwa ujumla. 



Mtaalam wa masuala ya Kijamii  Prof. David Mhando (kulia) pamoja na Mtaalm wa Mazingira Dr. Amina Hamad (kushoto) katika picha ya pamoja Prof. Ruwa-Aichi Temu mara baada ya  mazungumzo wakati wa kutathmini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya kiuchumi
















Post a Comment

0 Comments