Na: Adam Maruma.
Kaimu Mshauri wa Wanafunzi Chuo
Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA, Bi Hilda Gamuya, ameishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia msaada wa Vishikwambi (Tablet)
wanafunzi wenye uhitaji maalum wanaosoma mwaka wa kwanza katika Kozi mbalimbali
chuoni hapo ili viwasaidie kujifunza masomo yao kwa urahisi na kuendana na Kasi
ya wenzao darasani.
Baadhi ya wanafunzi hao walionufaika na msaada wa Vishikwambi wakiwa kwenye picha ya pamoja. |
Amesema kwa msaada huo ambao
Serikali imetoa ni jambo la kupongezwa, kwani kifaa hicho pamoja na kutumika
kutunzia kumbukumbu ya kinachofundishwa darasani pia wanafunzi hao watakua na
uwezo wa Kuongeza maarifa katika kusaka machapisho mengine kwenye mitandao
mingine ya kitaaluma kwa kile ambacho mwalimu atakua amekiwalisha kwa siku
husika.
Bi. Hilda Gamuya amesema msaada
huo haukuishia tu kwenye Vishikwambi kwani pia Serikali kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, imewapatia wanafunzi hao wenye changamoto mbalimbali
Bajaji 2 ambazo moja itakuwa Kampasi Kuu ya Edward Moringe na nyingine itakua
Kampasi ya Solomon Mahlangu, na zitatumika kwa usafiri kwa kundi hilo maalum
ili na wao wajione ni watu Muhimu katika
nchi yao na jamii inufaike kwa maarifa
ambayo SUA itawapatia kwa kipindi chote cha Masomo yao hapo Chuoni.
Mmoja wa Wanufaika wa msaada huo Zuhura
Ally ambae ni mwanafunzi wa mwaka wa
pili wa Shahada ya Ualimu chuoni hapo,
akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake huku akiongea kwa hisia
kali amesema wao kama wanufaika wa msaada huo, hawana cha kuilipa Serikali yao
pendwa Zaidi ya kumtakia Afya njema Rais Mh. Samia Suluhu Hassani ili aendelee
kuwaona wao kama kundi linalohitaji uangalizi wa karibu Zaidi kwa kuwa safari
yao ya kusaka elimu ina mengi ya kukatisha tamaa.
“Kuna kipindi niliwaza kuacha
masomo yangu hapa SUA, kwa sababu kila mwalimu akiingia darasani kufundisha
nakuwa na changamoto kuona hata nikikaa mbele nakuwa napishana na kile anachofundisha mwalimu hadi anamaliza
kipindi chote sielewi zaidi naona kama napoteza
muda wangu darasani, kwa kweli ilinikatisha tamaa nakuona ndoto yangu ya kuhitimu
Shahada yangu inakufa kwasababu naona safari yangu ya kimasomo hapa SUA,
inafikia mwisho wake, Lakini kwa vifaa hivi naanza kuona matumaini tena kwa
kweli nawashukuru sana na namtakia Afya njema Rais Samia Suluhu Hassan, kwa
vifaa hivi”, amesema Zuhura .
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Serikali ya wanafunzi SUASO, katika zoezi la ugawaji wa Vifaa hivyo Peter John ambae
ni Naibu Waziri wa Asasi Jinsia na Watu Wenye Mahitaji Maalum amesema Serikali
ya wanafunzi ya imeipongeza Serikali na SUA kwa ujumla kwa kuwajali wanafunzi
wenzao wenye Changamoto mbalimbali kwani na wao ni Binadamu na wanahitaji
kuungwa mkono kwa kufikia ngazi ya juu ya kutafuta elimu ya Chuo Kikuu.
PICHA MBALIMBALI ZIKIONESHA WANAFUNZI HAO WAKIKABIDHIWA VISHIKWAMBI.
0 Comments