SUAMEDIA

WAFUGAJI DODOMA KUNUFAIKA NA MAADHIMISHO YA TVA .

 Na: Adam Maruma.

Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kimepanga kufanya shughuli mbalimbali za kijamii mkoani Dodoma, ikiwa ni kuelekea katika Kongamano la Chama hicho litakalofanyika katika ukumbi wa Hazina mkoani humo kuanzia 5 Desemba, 2022.

Mwenyekiti wa TVA Prof. Esron Daniel Karimuribo akizungumza na SUAMEDIA ofisini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mwenyekiti wa Chama hicho cha Kitaaluma Prof. Esron Daniel Karimuribo amesema shughuli zitakazo fanyika  kwenye Tarafa ya Mbalawala nje kidogo ya Jiji la Dodoma  ni pamoja na huduma mbalimbali kwa wafugaji kama chanjo ya kuzuia homa ya mapafu kwa ngombe .

Prof. Karimuribo amezitaja chanjo nyingine zitakazotolewa katika wiki hiyo muhimu kwa Madaktari wa Mifugo kuwa  ni chanjo kwa ajili ya kuwakinga Mbuzi na Kondoo na ugonjwa wa Sotoka unaoshambulia wanyama hao pamoja na chanjo ya Mbwa, Paka na Punda kwa ajili ya Kuzuia ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa kwa wanyama hao.

Kwa upande wa Visumbufu vinavyosababisha magonjwa kwa mifugo kama kupe na mbun’go Chama hicho cha Madaktari wa Mifugo Tanzania, kimepanga kutoa elimu kwa wafugaji itakayowawezesha kupambana na visumbufu hivyo lakini pia kutakua na huduma ya kuogesha mifugo kwa kutumia josho linalotembea (mobile dip) ili kuweza kuwafikia wafugaji katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Mbalawala mkoani humo.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa suala la Elimu ya ufugaji bora na wenye tija kwa wafugaji na nchini kwa ujumla  litafikiwa endapo elimu ya ufugaji  itaanza kutolewa kwa  watoto hasa kwenye Taasisi kama Shule za Msingi na Sekondari na hivyo chama kimejipanga kutoa elimu hiyo  kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.

Prof. Karimuribo ameongeza kuwa suala la matumizi sahihi ya Dawa pia halijaachwa nyuma katika kushajihisha wiki hiyo na  amesema tatizo la matumizi holela ya dawa za kutibu mifugo inasababisha usugu wa vimelea vya magonjwa ambayo ni tatizo kubwa kwa wafugaji hivyo pia linapewa nafasi kubwa ya elimu kwa wafugaji hao.

Huduma nyingine ambayo Mwenyekiti huyo ameitaja ni huduma ya upasuaji kwa mifugo ili kuzuia  idadi ya mifugo kuzaliana kwa kasi  na kuongeza kuwa zoezi la hilo la upasuaji hufanyika ili kuondoa kizazi kwa mifugo jike  au kuhasi kwa  mifugo dume na pia upasuaji hufanyika kwa mifugo kama ng’ombe wanapokua wamekula mifuko ya plastiki ambayo haisagiki tumboni na hivyo kudhoofisha afya ya ngombe huyo, hivyo hupasuliwa na kutoa mfuko huo na afya ya mnyama huyo huimarika tena.

Aidha Prof. Karimuribo amesema Kongamano rasmi la Kisayansi litakua siku ya pili yaani tarehe 6 Desemba, 2022 ambalo linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa TAMISEMI Mh. Angela Kairuki na kutakua na mawasilisho  ya Tafiti mbalimbali za Kisayansi kwa mwaka Mzima kwa siku tatu mfululizo na litakamilishwa na Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania TVA.

Mwenyekiti huyo pia amewashukuru wadau mbalimbali watakaoshiriki kwenye maonesho ya vifaa tiba kwa mifugo, namna ya kutengeneza vyakula vya mifugo nje ya ukumbi wa kongamano hilo, pia amewashukuru wale waliowashika mikono kwenye shughuli hiyo kama vile Wizara ya Mifugo na Uvuvi,SUA,TAWIRI, na kampuni nyingine nyingi.

 

 

 


Post a Comment

0 Comments