SUAMEDIA

MHE. MWASA AWAOMBA WADAU WA MISITU NA MAZINGIRA KUUNGANISHA NGUVU

 Na: Calvin Gwabara

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amezipongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kulinda misitu na kutunza mazingira.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa akiongea na Waandishi wa habari na Maafisa wa TFCG na MJUMITA.

Pongezi hizo amezitoa wakati akiongea na Waandishi wa habari walioambatana na wakati viongozi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wanaotekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) walipokuwa kwenye ziara ya kutembelea vijiji vyenye miradi kuangalia mafanikio ya tangu ianzishwe pamoja na kuonana naviongozi kwenye mikoa na wilaya hizo.

“Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati kwakuwa unategemewa na taifa kwa mambo makuu matatu, Moja ni uzalishaji wa umeme wa maji kupitia bwawa la Kidatu linalochangaia asilimia 67% ya umeme wa maji nchini na litakapokamilika bwawa la Mwl. Nyerere Morogoro itachangia asilimia 93% ya Umeme wa maji Tanzania hivyo bila kuunganisha nguvu zetu tunaweza kukwamisha kufikia malengo”alisema Mhe. Mwasa.

Ametaja jambo linguine la kimkakati la mkoa wa Morogoro kuwa ni swala la maji mengi yanayotoka Morogoro kujaza mto Ruvu ambao maji yake yanategemewa Watanzania takribani milioni 11 wa Mkoa wa Morogoro,Pwani na Dar es salaam na kwamba Mto Ruvu ukikauka Dar es salaam inakuwa na shida ya maji.

Mhe. Mwasa amesema katika mambo hayo matatu makuu ya kimkakati lipo swala la uzalishaji wa chakula na kwamba Morogoro ndio mkoa wa Nne kwa uzalishaji lakini ni Mkoa wa Kwanza kwa uzalishaji wa Mpunga Tanzania,wa kwanza kwa uzalishaji wa Sukari na wa sita kwa uzalishai wa Ndizi lakini uhaba wa mchele nchini unaopelekea kufika kilo moja kwa shilingi 3,000/- ni matokeo ya uharibifu wa misitu na kukosa mvua za kutosha.

Amesema changamoto kubwa ambazo Mkoa unapambana nazo ni Ukataji wa miti hovyo kwa matumizi ya binadamu,Uchomaji misitu,Mifugo  pamoja na uchomaji wa mkaa bila kufuata taratibu na hivyo kuteketeza misitu mbalimbali iliyo kwenye ardhi za vijiji.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro amesema hivi sasa wamedhamiria kuzuia ukataji wa misitu usiozingatia taratibu wala vibali na tayari wameshakaa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuona uwezekano wa kumalizia wale walio na vibali na kisha kusitisha vibali kwa kujipa muda na kutafakari namna ya kupanda miti kwenye maeneo yaliyoharibiwa badala ya kuchoma mikaa isiyo rasmi.

Mhe. Mwasa amesema zoezi hilo litakwenda sambamba na kufanya kampeni ya matumizi ya Nishati safi yaani Umeme na Gesi ili kupunguza matumizi ya mkaa kwani asilimia 50% ya Mkaa unazalishwa Morogoro unatumiwa na Jiji la Dar es salaam ambao watu wake ni wa uchumi wa kati wenye uwezo wa kumudu kutumia Gesi na umeme endapo itafanyika kampeni ya uhamasishaji vizuri.

“Matumizi ya gesi ni rahisi zaidi kuliko Mkaa ni kubadili fikra tuu kuwa gesi ni ghali na hatari na kwangu mimi heri ianyetumia kuni kuliko mkaa maana ili kupata tani moja ya mkaa unahitaji kuteketeza miti tani saba hadi nane sasa mkaa ni uharibifu mkubwa wa mazingira kuliko tunavyodhani inatakiwa mtu akiona gunia la mkaa mwili wote usisimke ajihisi na kuona tunakufa kama nchi”alifafanua Mwasa.

Amesema wamepewa maagizo kumi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania Mhe. Philip Mpango hivyo wanakaa na Wakuu wa wilaya,Wakurugenzi na Maafisa mistu wenyewe mkoa Mzima kueleza namna gani wanakwenda kutekeleza maagizo hayo.

Mradi wa CoForEST unatekelezwa katika vijiji 41 vilivyopo kwenye wilaya za Morogoro, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro, Liwale, Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi na Kilolo mkoani Iringa.

PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI OFISINI KWA MKUU WA MKOA KABLA NA BAADA YA MKUTANO HUO.







 



Post a Comment

0 Comments