SUAMEDIA

Mwanafunzi wa (SUA) ashinda Uandishi wa Insha Afrika

                                            

Na: Winifrida Mwakalobo

Mwanafunzi wa mwaka wa Tatu, Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Mazingira katika Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo  Bw. Innocent James ameishukuru Menejimenti ya Chuo kwa kutambua mchango wake katika Uandishi wa Insha mara baada ya kuibuka kuwa mshindi wa pili barani Afrika.

Mwanafunzi wa mwaka wa Tatu, Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Mazingira katika Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo  Bw. Innocent James akipokea Tuzo kutoka kwa Menejimenti ya Chuo kwa kutambua mchango wake katika Uandishi wa Insha mara baada ya kuibuka kuwa mshindi. (Picha na Gojo Mohamed.)

Amebainisha hayo mara baada ya kutunukiwa cheti pamoja na tuzo na mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Othman Chande katika Mkutano wa 170 wa Baraza la Chuo uliofanyika hivi karibini katika ukumbi wa Baraza chuoni hapo.

Amesema kuwa Cheti pamoja na Tuzo aliyopatiwa na Menejimenti ya SUA imempa hamasa na kuwafanya wengine wahamasike zaidi katika kushiriki kwenye fursa mbalimbali ambazo zinajitokeza na kukitangaza Chuo na Taifa kwa ujumla.

‘‘Nipende kuwahimiza vijana wenzangu hasa wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati nchini kutenga muda wao kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano mbalimbali kama haya kwa kuwa wanapata kujifunza mambo mbalimbali na kuweza kupanua uelewa wao na kuwapatia mambo tofauti ambayo ni muhimu  katika taaluma zao,’’ amesema Bw. Innocent James

Aidha Innocent amesema alichojifunza katika mashindano hayo ni kutokata tamaa kwa kuwa amejaribu kuandika Insha zaidi ya mara mbili tangu akiwa mwaka wa kwanza 2019/2020 na mwaka wa pili 2020/2021 ambapo hakuweza kufanikiwa kushinda na alipojaribu kwa mara ya tatu 2021/2022 akiwa mwaka wa tatu ndipo amefanikiwa kushinda hivyo amewataka vijana wenzake kutokata tamaa na kuendelea kujaribu ili kufikia malengo yao. 

Mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Shirika la Viwango Afrika (ARSO) na kuratibiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) yenye kauli mbiu isemayo ‘‘Kutafakari Mchango wa Viwango katika Kuendeleza Uchumi wa Viwanda Hususani Kwenye Sekta ya Madawa na Vifaa Tiba Dhidi ya Mapambano ya Ugonjwa wa UVIKO 19  ambao umekuwa tishio kwa Nchi za Afrika na Duniani kwa Ujumla Pamoja na Magonjwa Mengine’’.

                                                                                                  






KATIKA VIDEO

Post a Comment

0 Comments